MANCHESTER, Uingereza
HATIMAYE kocha Michael Carrick amefutwa kazi pale Old Trafford na anaiacha Manchester United ikiwa kwenye nafasi za chini kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England msimu huu wa 2026-27.
Taarifa za kuondoka kwake zimekuja baada ya Man United kushangilia sare ya mabao 4-4 dhidi ya Aston Villa, mchezo ambao walikuwa kwenye hatua za mwisho za kuupoteza.
Chini ya Carrick, timu hiyo imepata ushindi wa mechi moja pekee kati ya 10 za Ligi, mwenendo uliowashitua mabosi na kuona huenda hali ikawa mbaya zaidi endapo wataendelea kumsikilizia.
Ni miezi takribani 10 tu tangu mabosi wa Man United walipompa mkataba wa kudumu baada ya kufanya vizuri akiwa kocha wa muda? Nini kilichomwangusha kiungo huyo wa zamani?
SAFARI YA MATUMAINI
Baada ya kuajiriwa kama kocha wa muda, Carrick alianza vizuri kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Man City, kisha akapata ushindi mbele ya timu kubwa tatu za jijini London; Arsenal, Fulham na Tottenham.
Man United iliyoonekana imepotea ikiwa na kocha Ruben Amorim, ikashinda mechi nne mfululizo za Ligi kwa mara ya kwanza tangu ilipofanya hivyo miaka miwili iliyopita.
Akiwa ameikuta timu ikiwa nafasi ya saba, Carrick akamaliza msimu ndani ya ‘Top 3’ na Man United kurejea kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa kipindi alichokaa kwenye benchi, kuanzia Januari hadi msimu unakwisha, Man United ikawa imekusanya pointi nyingi {39] kuliko mabingwa Arsenal akiwa ameshinda mechi 12 kati ya 17 za Ligi.
MAJANGA YALIANZIA HAPA
Hata kabla ya mechi ya kumaliza msimu dhidi ya Brighton, Carrick akapewa ajira ya kudumu. Katika dirisha kubwa hilo la usajili, mabosi wa Man United walitumia Pauni milioni 163 tu kwenye usajili.
Ni kiasi kidogo cha fedha, ukilinganisha na kilichotumiwa na klabu ngeni kwenye Ligi, Hull City na Ipswich Town. Badala ya kuimarisha ulinzi na ushambuliaji, zikatumika fedha nyingi kusajili viungo Youri Tielemans, Andrey Santos na Carlos Baleba aliyetua akiwa majeruhi.
Dalili mbaya zilianza kujitokeza katika mechi ya ufunguzi wa msimu wa 2026-27 baada ya Man United kutandikwa na Hull City. Upepo mbaya ukaiandama timu hiyo kuanzia hapo na kujikuta ikiambulia pointi saba pekee katika mechi saba za mwanzo.
Wakati mambo yakiwa hayaendi vizuri, hasa baada ya Man United kufungwa na Atletico Madrid katika mechi ya Ligi ya Mabingwa, beki Lisandro Martinez akazua gumzo baada ya kumpa ‘makavu’ Mkurugenzi wa ufundi, Jason Wilcox.
“Tulikuwa vizuri msimu uliopita, hivyo tulitarajia kuendelea kuwa juu kwa kusajili wachezaji wa kuongeza ushindani kwa sababu timu nyingi zimesajili wachezaji wazuri,” alisema.


