JERUSALEM, Palestina
ACHILIA mbali tabu wanazopitia, ikiwamo kuishi kwenye mahema kwa kukosa makazi, raia wa Palestina wanaoishi Ukanda wa Gaza wamekumbwa na mafuriko yaliyosabishwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Umoja wa Mataifa, wakazi wa eneo hilo wanahitaji msaada kutokana na kadhia hiyo.
Katika picha na video zilizosambaa, wakazi wa Gaza wanaonekana wakijaribu kuondosha maji yaliyojaa kwenye mahema yao,
Mwakilishi wa Shirika la Watoto la Kimataifa [UNICEF], Jonathan Veitch, amesema hali imekuwa mbaya zaidi baada ya Israel kuzuia vifaa vya kudhibiti mafuriko kuingia Gaza.
Asilimia 90 ya raia wa Palestina hawana makazi kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Israel na Hamas.
Aidha, mafuriko ya sasa yametajwa kuharibu kabisa mahema takribani 70,000 ya wakazi hao katika eneo la Gaza.


