12.9 C
New York

Mkuyu Africa kufungua fursa za uwekezaji kupitia Russia -Africa Summit

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini-Moscow

KAMPUNI ya Mkuyu Africa imeeleza dhamira ya kupanua wigo wa biashara na kufungua fursa mpya za uwekezaji baada ya kushiriki mazungumzo ya kibiashara yaliyowakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na wawekezaji kutoka Urusi jijini Moscow.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Hoteli ya Four Seasons, pembezoni mwa Mkutano wa Russia–Africa Summit, yalilenga kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi, hususan katika sekta za nishati, kilimo, madini, ujenzi na miundombinu.

Ujumbe wa Tanzania, uliowajumuisha wawakilishi wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na wafanyabiashara kutoka sekta mbalimbali, ulitumia jukwaa hilo kueleza fursa zilizopo nchini na kuhamasisha wawekezaji wa Urusi kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.

Akizungumza baada ya mkutano huo, Mkurugenzi wa Mkuyu Africa, Juneid Othman, alisema ushiriki wao umefungua nafasi ya kujenga mahusiano mapya ya kibiashara, kubadilishana uzoefu na kukutana na wawekezaji wanaoweza kusaidia kukuza shughuli za kampuni.

“Tumefurahi kushiriki katika mkutano huu mkubwa wa uwekezaji kwa sababu umetupa nafasi ya kukutana na wafanyabiashara mbalimbali, kujifunza kutoka kwao na kujenga mahusiano yatakayoweza kutusaidia kupanua wigo wa biashara zetu,” alisema Juneid.

Mkuyu Africa inajihusisha na uuzaji, upangishaji na ujenzi wa majengo ya makazi na biashara nchini Tanzania, ikiwa na miradi katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, yakiwemo Kariakoo, Masaki, Msasani, Kawe, Mbezi na Mikocheni.

Kupitia shughuli hizo, kampuni inalenga kuchangia maendeleo ya sekta ya majengo, kuhamasisha umiliki wa mali na kukuza uwekezaji katika biashara zinazohusiana na ujenzi.

Kwa upande wake, mfanyabiashara kutoka Kenya, Peter Omong, alisema mikutano ya kimataifa ya uwekezaji ni fursa muhimu kwa wafanyabiashara, hasa vijana, kupata washirika na kupanua mitandao yao ya kibiashara.

Omong alisema kupitia mkutano huo amepata mahusiano mapya, yakiwemo fursa katika biashara ya mafuta mazito na mbolea, ambazo ana matumaini zitasaidia kupanua shughuli zake.

Ushiriki wa wafanyabiashara wa Tanzania katika majukwaa hayo unaweka nafasi ya kutafuta masoko mapya, kuvutia mitaji na kuanzisha ushirikiano unaoweza kuchochea ukuaji wa biashara na uwekezaji nchini.

Related articles

Recent articles