21.3 C
New York

Watoto wa wanasoka wanaofuata nyayo za wazee zao

Published:

LONDON, Uingereza

MAJI hufuata mkondo! Ni msemo maarufu na uliojidhirisha wazi katika ulimwengu wa soka kwa baadhi ya wanasoka waliostaafu kurithisha vipaji kwa watoto wao.

Kwa sasa, soka la England linaye Reggie Watson. Kiungo huyo wa Chelsea ana umri wa miaka 16 na ni mtoto wa mkongwe wa kikosi cha Wigan kilichotwaa taji la FA mwaka 2013, Ben Watson.

Wakati huo huo, kuna Jack na Tyler, watoto wa kiungo wa zamani wa Manchester United, Darren Fletcher. Nao wako United na Jack [19] alicheza mechi tatu za Ligi Kuu ya England msimu uliopita, wakati Tyler [16] ameshuka dimbani mara mbili.

Aidha, straika wa zamani wa Arsenal, Robin van Persie, anaye mtoto wake aitwaye Shaqueel. Dogo huyo ana miaka 19 na anacheza Feyenoord, klabu ya Uholanzi aliyowahi kucheza baba yake.

Kama alivyokuwa baba yake, Shaqueel naye anacheza eneo la mshambuliaji wa kati na alifunga mabao mawili katika mechi tatu za msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Uholanzi [Eredivisie].

Mkongwe wa Liverpool, Emile Heskey, ana watoto wake wawili wanaocheza soka. Wote walianzia Manchester City lakini Reigan [18] amejiunga na Cologne ya Ujerumani.

Kwa upande wake, Jaden [20], bado yuko Man City, ingawa ameendelea kucheza kwa mkopo Sheffield Wednesday, klabu ambayo aliitumikia pia msimu uliopita.

Aidha, straika wa zamani wa AC Milan, Zlatan Ibrahimovic, pia anao vijana wake wawili, Maximilian na Vincent. Maximilian [19], anacheza AZ ya Uholanzi, wakati mdogo wake, Vincent [18] anakipiga AC Milan.

Mbali na hao, kuna Kai Rooney. Mtoto wa mkongwe wa Man United na timu ya taifa ya England, Wayne. Kai [16], anacheza eneo la straika katika timu ya vijana wa U-18 pale Old Trafford.

Sambamba na hao, yupo pia Gabriel, kijana wa kocha wa Arsenal, Mikel Arteta. Kinda huyo wa miaka 17, yuko pale Emirates na amekuwa akitumika katika timu ya vijana ya U-18.

Vipi kuhusu Cristiano Jr? Ni mtoto wa supastaa wa soka la Ureno, Cristiano Ronaldo. Cristiano Jr anayecheza eneo la ushambuliaji, ana umri wa miaka 16 na tayari ameonesha uwezo mkubwa wa kuzipasia nyavu.

Kinda huyo amekuwa akiongozana na baba yake katika klabu zote, akianzia Man United, Juventus na sasa ni sehemu ya ‘academy’ ya Al-Nassr huko Saudi Arabia.

Related articles

Recent articles