Na mwandishi wetu, Gazetini
SHIRIKA la Watoto la Umoja wa Mataifa [UNICEF] limefanya utafiti wake na kubaini ongezeko kubwa la vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya vijana wenye umri mdogo.
Kupitia utafiti huo uliohusisha vijana 21,000, UNICEF imebaini kuwa katika kila watoto watano wenye umri kati ya miaka 12 hadi 17, basi mmoja amewahi kudhalilishwa kingono huko mitandaoni.
Kwa kipindi cha mwaka mmoja, utafiti umeeleza pia kwamba watoto zaidi ya milioni 15 wamekumbana na unyanyaji wa kingono katika mitandao mbalimbali.
Kati yao, milioni 9 walipewa msukumo wa kuingia kwenye mazungumzo ya kingono, kutuma picha za utupu na wengine milioni nne walitumiwa pasi na ridhaa yao.
Mbaya zaidi, asilimia 41 ya watoto wanaokumbana na vitendo hivyo vya kunyanyaswa kingono wamekuwa wakificha kusimulia na ni asilima chini ya moja walioweza kuripoti kwa mamlaka husika.
Inashangaza pia kuona idadi kubwa [57%] ya wanaofanya vitendo hivyo wanawafahamu watoto wanaowalenga, kwamba kama si mafariki na ndugu, basi ni wapenzi wao.
Ni kwa matokeo hayo, UNICEF inaamini kuwa mitandao si sehemu salama kwa watoto au vijana wadogo na kama watatumia, basi lazima wawe chini ya uangazi wa wazazi/walezi.
Wakati huo huo, utafiti umebaini kuwa matumizi ya mtandao yamechagiza kwa kiasi kikubwa changamoto za kisaikolojia, ikiwamo matatizo ya afya ya akili, kwa makundi hayo na wakati mwingine kuzalisha matukio ya kujiua.
Nchini Marekani hivi karibuni, kampuni ya Meta inayomiliki mitandao ya kijamii ya Instagram na Facebook ililazimika kulipa fidia baada ya kufunguliwa mashitaka ya maudhui yake kuharibu saikolojia za watumiaji wake wenye umri mdogo.
Hata utafiti wa UNICEF unaeleza kuwa asilimia 60 ya vitendo vya unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto hufanywa kupitia Facebook, WhatsApp na Instagram, ambao pia unamilikiwa na Meta, ikifuatiwa na Snapchat, TikTok na YouTube.
Majimbo kadhaa yalifungua kesi Oakland, California, yakiishitaki Meta kwa kuwaharibu watoto na hatimaye kampuni hiyo kukubali kulipa fidia ya Dola za Marekani bilioni 17.1.
Sambamba na kulipa fidia, pia Meta ilikubali kuweka utaratibu wa watoto kuingia mitandaoni kwa dakika 120 tu kwa siku, pia kuwaondoshea kabisa huduma kwa nyakati za usiku.
Desemba, 2025, katika kudhibiti athari, hasa kwa watoto, Australia ilikuwa nchi ya kwanza duniani kuweka zuio la mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 16 kumiliki akaunti ya YouTube, X [twitter], Facebook, Instagram, TikTok na Snapchat.
Ufaransa ilikuwa nchi ya kwanza ya Umoja wa Ulaya [EU] kupiga marufuku kijana mwenye umri chini ya miaka 15 kutumia mitandao ya kijamii, ingawa bado kuna mvutano kwa madai kuwa inakinzana na uhuru wa kujieleza. UK itaanza utekelezaji wa sheria ya aina hiyo ifikapo mwaka 2027.


