Na mwandishi wetu, Gazetini
MSIMU huu wa 2026-27 wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika utaanza wikiendi hii, Septemba 4-6, 2026, ambapo zitachezwa mechi za hatua ya awali ya raundi ya kwanza.
Jumla ya klabu 61 zinashiriki msimu huu, huku Mamelodi Sundowns ikijaribu kutetea taji ililobeba msimu uliopita. Hata timu itakayoishia hatua hii ya awali, bado itapokea kitita cha Dola 100,000 [zaidi ya Sh Mil. 264 za Tanzania].
Wikiendi hii, mabingwa mara tano kwenye mashindano hayo, TP Mazembe, watakuwa ugenini kukabiliana na vigogo wa Ligi Kuu ya Ghana, Medeama SC.
Mshindi wa matokeo ya jumla baada ya marudiano wiki moja baadaye ataumana na Club Africain ya Tunisia au Djoliba AC ya Mali katika hatua inayofuata.
Wakongwe wa soka la Misri, Zamalek, wao pia wataanzia ugenini kwa kuifuata AS Port ya Djibouti. Wenzao wa Misri, Pyramids FC, watakuwa Nairobi kuivaa Gor Mahia.
Orlando Pirates ya Afrika Kusini itakuwa Mauritius kucheza na La Cure Waves inayoshiriki kwa mara ya kwanza mashindano hayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Mshindi atakabiliana na aidha AS Mangasport [Gabon] au African Stars [Namibia].
Wakati huo huo, macho ya wapenzi wa soka la Afrika Mashariki yatakuwa zaidi kwa klabu kongwe za Tanzania, Simba na Yanga, ambazo nazo zitashuka dimbani wikiendi hii.
Simba, kwa upande wao, watakuwa na kibarua nchini Malawi, ambako watakwaana na Mighty Wanderers, wakati Yanga watakiwasha na mabingwa wa Ligi Kuu ya Botswana, Gaborone United.
Katika mechi zingine kali, vigogo wa soka la Ivory Coast, ASEC Mimosas, watacheza dhidi ya ASCK ya Togo, Al Hilal ya Sudan itakwaana na Aigle Noir ya Burundi, huku Atlético Petro de Luanda ya Angola itasafiri hadi Msumbiji kuifuata UD do Songo.


