20.9 C
New York

Dili za ‘bei mbaya’ usajili wa kiangazi Ulaya 2026

Published:

LONDON, Uingereza

HATIMAYE usajili wa majira ya kiangazi kwa mwaka 2026 ulifungwa rasmi juzi, Septemba 1, huku Enzo Fernandez aliyeondoka Chelsea akiwa ndiye mchezaji ghali zaidi safari hii.

Enzo ametua Manchester City, huku dili hilo likiipatia Chelsea kitita cha euro milioni 145, wakati huo pia Blues wakimsajili Morgan Rogers ambaye ameshika nafasi ya pili nyuma ya Muargentia huyo.

Rogers anayecheza eneo la kiungo mshambuliaji ameigharimu Chelsea euro milioni 138 akitokea Aston Villa. Mchezaji ambaye msimu uliopita alifunga mabao 10 na kutoa ‘asisti’ sita.

Mchezaji aliyeshika nafasi ya tatu ni kiungo Elliot Anderson aliyetua Manchester City kwa euro milioni 135 akitokea Nottingham Forest, akifuatiwa na Bradley Barcola aliyetua Liverpool kwa euro milioni 125 akitokea PSG.

Katika nafasi ya tano ni kiungo mpya wa Tottenham aliyetokea Newcastle United, Sandro Tonali, ambaye usajili wake umegharimu euro milioni 108.

Kiungo mwingine, Mateus Fernandes, anafuata katika nafasi ya sita baada ya usajili wake wa kutua Tottenham akitokea Southampton kugharimu kitita cha euro milioni 99.

Anafuatiwa na winga kutoka Lille, Ayyoub Bouaddi, aliyetua Manchester City kwa ada ya euro milioni 95, kisha Savio aliyesajiliwa na Tottenham akitokea Etihad kwa euro milioni 87.

Wengine ni kiungo wa Arsenal kutoka Newcastle United, Bruno Guimaraes, ambaye usajili wake umewagharimu Washika Bunduki hao wa London kiasi cha euro milioni 87.5.

Anayekamilisha ‘Top 10’ ni kiungo aliyetoka Brighton na kujiunga na Manchester United, Carlos Baleba. Usajili wa nyota huyo raia wa Cameroon umegharimu euro milioni 75.9.

Related articles

Recent articles