QUITO, Ecuador
RAIS wa zamani wa Ecuador, Lenín Moreno, amehukumiwa kifungo cha miaka mitano gerezani baada ya kukutwa na hatia katika mashitaka ya rushwa.
Mwanasiasa huyo aliyeiongoza Ecuador kati ya mwaka 2017 hadi 2021, anakuwa rais wa tatu wa zamani wa Ecuador kuhukumiwa kwa mashitaka ya aina hiyo.
Aidha, hukumu hiyo imewaangukia pia mkewe, binti yake na kaka yake, wakihusishwa kulipwa fedha na kampuni ya Kichina iliyotekeleza mradi wa umeme nchini humo.
Waendesha mashitaka wamedai kuwa kampuni hiyo, Sinohydro, ililipa Dola milioni 76.1 kwa vigogo wa Serikali ya Ecuador, akiwamo Moreno na familia yake hiyo.
Hata hivyo, kutokana na umri wake mkubwa na wa miaka 73, wanasiasa huyo atatumikia kifungo cha ndani na si kwenda jela.
Kwa upande mwingine, ameahidi kuchukua hatua ya kukata rufaa ya kupinga hukumu hiyo inayowahusisha pia wenzake 19.


