Na mwandishi wetu, Gazetini
NI moja ya sekta muhimu yenye fursa kubwa ya kuchangia maendeleo ya nchi. Hii inatokana na utajiri wa rasilimali za madini, zikiwemo dhahabu, almasi, tanzanite, na madini ya kimkakati kama grafiti, lithium, urani, na madini adimu.
Madini haya yanazidi kupata umuhimu na thamani kubwa, wakati ambapo sekta ya nishati duniani inabadilika kuelekea nishati safi na kutumia teknolojia ambazo zinachangia uhifadhi wa mazingira.
Katika miongo ijayo, sekta ya madini itakuwa na mchango mkubwa katika kukuza Pato la Taifa, kufungua fursa za ajira, kuongeza mauzo ya nje na kuhaulisha teknolojia ya madini.
Wakati huo huo, itachochea ukuaji wa sekta zingine kama vile za ujenzi, viwanda na nishati.
Hata hivyo, ili kupata manufaa ya muda mrefu kutokanana na sekta hii, ni muhimu kuwa na mbinu endelevu za uchimbaji wa madini, kanuni za wazi za usimamizi na uwekezaji katika teknolojia muafaka.
Kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya madini kutasaidia kuzalisha ajira na kuongeza mapato ya mauzo ya nje, hivyo kuimarisha mchango wa sekta hii kwa uchumi wa Taifa.


