MIAMI, Marekani
SAHAU kabisa kuhusu matokeo. Fainali ya Kombe la Dunia iliyochezwa jana iliwakutanisha makocha wawili, Luis de la Fuente wa Hispania na Lionel Scaloni anayeinoa Argentina.
Ukiweka kando ubora wa mbinu na mafanikio yao, kuna stori nyingine ya kufurahisha kuhusu wawili hao.
Stori yao hiyo inaanzia mwaka 2017, ambapo Scaloni alikuwa Hispania na kuhudhuria masomo ya ukocha ya leseni ya Uefa Pro. Ndiyo ngazi ya juu zaidi katika taalamu hiyo barani Ulaya.
Akiwa darasani, mmoja ya waalimu wake alikuwa De la Fuente, ambaye pia wakati huo alikuwa kocha wa U-19 ya Hispania.
De la Fuente (65), alikuwa mwalimu wa somo la mbinu za soka, ambalo Scaloni alikuja kufaulu kwa alama za juu.
Tangu hapo, wawili hao wakainza safari ya urafiki mkubwa uliodumu hadi leo hii.
Katika mchezo wa jana, walikutana wakiwa na mafanikio makubwa. De la Fuente aliiongoza Hispania kutwaa taji la EURO 2024, wakati Scaloni aliipa Argentina ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2022.
Ni makocha ambapo licha ya mafanikio hayo kwenye timu za taifa, hakuna aliyewahi kuinoa klabu kubwa ya soka barani Ulaya.
Katika soka, De la Fuente alistaafu kucheza mwaka 1994 na baadaye kuinoa Deportivo Alaves iliyomfuta kazi mwaka 2011.
Akiwa nje ya kazi kwa miezi 18, hatimaye alituma maombi na kisha kuajiriwa kuinoa timu ya U-19 ya Hispania.
Ndani ya miezi mitatu kazini, akiiwezesha kufika nusu fainali ya EURO ya vijana, akiweza kuibua vipaji vya Rodri, Unai Simon na Mikel Merino, ambao walimpa ubingwa wa michuano hiyo msimu uliofuata.
Kutokana na mafanikio yake akiwa na U-19 na baadaye U-21, De la Fuente alipewa timu ya wakubwa ya Hispania mwaka 2022.
Kwa sasa, mtoto wake wa kiume aitwaye Alberto ni miongoni mwa makocha wasaidizi kwenye benchi la ufundi la Hispania.
Scaloni, kwa upande wake, alizaliwa katika mji mdogo wa Pujato, jirani na Rosario anakotokea nahodha wake, Lionel Messi.
Tangu akiwa mdogo, baba yake alikuwa na kawaida ya kuwachukua Scaloni na kaka yake, Mauro, na kuwapeleka katika viwanja vya soka.
Baadaye, Scaloni aliingia kwenye U-20 ya Argentina iliyotwaa Kombe la Dunia la vijana mwaka 1997.
Ni kikosi kilichochukua na makinda wengi waliokuja kuwa mastaa, wakiwamo Walter Samuel na Pablo Aimar, ambao kwa sasa ni wasaidizi wake kwenye benchi.
Akiwa kinda wa Deportivo La Coruna ya Hispania, Scaloni alizoeleka kwa kusafiri mara kwa mara na baba yake kwenye mechi zao.
Angetumia basi la wachezaji wakati wa kwenda kwenye mechi, kisha angerudi nyumbani na baba yake wakiwa na usafiri binafsi.
Akiwa amecheza mechi zaidi ya 200 na kunyakua ubingwa wa La Liga, Scaloni aliondoka Deportivo na kuzitumikia klabu mbalimbali, ikiwamo West Ham United.
Alistaafu kucheza soka msimu wa 2014-15, kisha kazi yake ya kwanza ya ukocha ikaja mwaka 2016 akiwa msaidizi wa Jorge Sampaoli katika benchi la Sevilla.
Mwaka mmoja tu baadaye, wawili hao waliteuliwa kuliongoza benchi la ufundi la Argentina.
Hata hivyo, Sampaoli alifukuzwa mwaka 2018 baada ya Argentina kufanya vibaya kwenye fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Urusi.
Chama cha Soka cha Argentina kilipomtangaza Scaloni kuchukua nafasi yake, wengi walikosoa, wakisema kocha huyo hana uzoefu wa kutosha.
Licha ya ukosolewaji huo, alijibu kwa vitendo kwa kutwaa Copa America mwaka 2021, taji la kwanza kwa Messi akiwa na timu ya taifa, kisha akabeba Kombe la Dunia (2022).


