DAKAR, Senegal
KOCHA wa timu ya soka ya Taifa ya Senegal, Pape Thiaw, ameondoshwa kwenye majukumu hayo zikiwa ni siku chache tu tangu walipotolewa Kombe la Dunia.
Senegal iliishia hatua ya 32 Bora baada ya kufungwa mabao 3-2 na Ubelgiji. Katika hatua ya makundi, walifungwa mechi mbili za awali, kabla ya kuifunga Iraq mabao 5-0.
Baada ya kutolewa, kiungo wa timu hiyo, Pape Gueye, alisema ataacha kuzitumikia endapo benchi la ufundi litaendelea kufanya kazi.
Katika taarifa yake, Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) limedai kuwa limepitia mwenendo wa timu hiyo na kufikia uamuzi wa kumtimua kocha.
Thiaw ndiye aliyekuwa kocha wakati Senegal inatwaa taji la AFCON mwaka 2025, kabla ya kupokonywa ubingwa na kupewa Morocco waliokutana nao fainali.
Adhabu hiyo ilitokana na Thiaw na wachezaji wake kutoka nje ya uwanja siku ya fainali ili kugomea penalti waliyopewa Morocco katika mchezo huo.
Kwa sasa, FSF wanasubiri majibu ya rufaa waliyokata CAS (Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi Michezoni) kupinga hatua ya kupokonywa ubingwa.


