LONDON, Uingereza
MKONGWE Alan Shearer ametaja ‘first eleven’ inayoweza kuipa ubingwa wa msimu wa Kombe la Dunia timu ya soka ya Taifa ya England.
England chini ya kocha raia wa Ujerumani, Thomas Tuchel, imeshavuka Kundi L na kutinga hatua inayofuata ya 32 Bora.
Walianza mashindano hayo kwa ushindi wa mabao 4-2, kisha suluhu (0-0) dhidi ya Ghana, kabla ya kuitandika Panama.
Kwa upande wake, Shearer mwenye umri wa miaka 55, ametaja kikosi cha kwanza anachoamini kitaipa timu hiyo taji la msimu huu, akianza na kipa Jordan Pickford.
Katika safu ya ulinzi, lejendari huyo amewapanga Reece James, John Stones, Marc Guehi na Nico O’Reilly.
Eneo la kiungo katika kikosi chake lina Elliot Anderson, Declan Rice na Jude Bellingham, wakati Bukayo Saka na Marcus Rashford wakitokea pembeni, huku Harry Kane akisimama juu (straika).


