18.2 C
New York

Siasa za Afrika na kitendawili cha demokrasia

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

KWA miaka ya hivi karibuni, baada ya kufuatilia chaguzi za Afrika, wachambuzi wa siasa wameibua kile wanachokiita mdororo wa afya ya demokrasia barani humu.

Chaguzi zilizoharibiwa na sura za vitendo vya rushwa, hali ya usalama isiyoridhisha, ukandamizwaji wa uhuru wa kujieleza, vyama vya siasa kubanwa mbavu, na vita mpya kati ya vijana wa GEN Z na mifumo ya uongozi katika nchi zao.

Uchaguzi ulioko kwenye mijadala ya siasa kwa sasa ni ule wa Ethiopia, ambapo umefanyika wakati baadhi ya maeneo ya nchi hiyo, ukiwamo Mkoa wa Tigray, yakitawaliwa na vurugu.

Tigray haijashiriki Uchaguzi kwa mwaka wa sita sasa kutokana na mapigano yake na wanajeshi wa Serikali yaliyoanza mwaka 2020. Ikumbukwe, Tigray inashinikiza mamlaka kamili, hivyo haiiungi mkono Serikali iliyoko madarakani.

Wakati huo huo, Serikali inakosolewa vikali kwa kukandamiza wapinzani kwa lengo la kukipa Chama tawala nafasi ya kubaki madarakani.

Tukitoka huko na kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Zambia utakaofanyika Agosti, 2026, mazingira magumu ya uhuru wa kujieleza hayatofautiani sana na Ethiopia.

Wanaharakati wa vyombo vya habari hawaoni vituo vya redio, televisheni na magazeti vikiwa na uhuru wa kufanya kazi zao pasi na kuingiliwa na mamlaka, ikiwamo kupangiwa nini cha kuripoti.

Aidha, ni wiki chache tu zimepita tangu Rais Yoweri Museveni alipoapishwa kurudi madarakani, akiiongoza Uganda tangu mwaka 1986.

Mbaya zaidi, ushindi wake umegubikwa na madoa ya kila aina, kuanzia kuvikalia kooni vyombo vya habari, kuwapa wakati mgumu wanasiasa wa upinzani, hadi vyombo vya dola kushutumiwa kwa matumizi makubwa ya nguvu dhidi ya raia.

Kwa upande wa Magharibi mwa Afrika, kiongozi wa kijeshi, Ibrahim Traore, ambaye aliingia madarakani kwa mapinduzi ya mwaka 2022 nchini Burkina Faso, alitoa kauli nzito Aprili, 2026, alipowaambia wananchi wa Taifa hilo kusahau kuhusu demokrasia.

Katika kauli yake iliyoibua mitazamo tofauti, Traore alisema demokrasia imekuwa ikisababisha machafuko na mauaji barani Afrika, hivyo haipaswi kupewa nafasi.

Wapo waliopinga na wengine kusema kiongozi huyo yuko sahihi, kwamba demokrasia ni mfumo wa wakoloni uliolenga kuondosha umoja, amani na utulivu katika mataifa ya ‘dunia ya tatu’.

Mataifa jirani ya Mali, Niger, Gabon, Chad, Guinea na Guinea-Bissau nayo yakaingia kwenye tawala za kijeshi kwa nyakati tofauti.

Niger, Mali na Burkina Faso zikajitoa Jumuhiya ya Uchumi kwa Mataifa ya Kusini mwa Jangwa la Sahara (ECOWAS) na kuunda Umoja wao wa Alliance of Sahel States (AES).

Related articles

Recent articles