25.9 C
New York

Uholanzi ilivyofanikiwa mfumo wa elimu, ajira kwa vijana

Published:

AMSTERDAM, Uholanzi

KWA mujibu wa sheria za Uholanzi, ni lazima kwa watoto wenye umri kati ya miaka mitano hadi 16 kuwa shuleni. Pia, ni lazima kubaki shule au kwenye mafunzo ya ufundi hadi watakapotunukiwa vyeti au kutimiza umri wa miaka 18.

Kuanzia umri wa miaka 12, mwanafunzi atapita moja kati ya njia tatu za kusoma elimu ya sekondari. Njia hiyo itategemea na matokeo ya mtihani au mapendekezo ya mwalimu.

Njia ya kwanza ni ‘VMBO’, masomo yanayompeleka elimu ya ufundi. Njia ya pili ni ‘HAVO’, ambayo itampeleka katika masomo ya sayansi. Njia ya tatu ni ‘VWO’, yaani masomo yatakayompeleka katika vyuo vikuu vya tafiti.

Hata hivyo, wakosoaji wa mfumo huo wamekuwa wakieleza wasiwasi wao juu ya uwezo wa watoto wenye umri mdogo kuchagua kitu sahihi kitakachowasaidia maishani.

Mathalan, Amelie akiwa na umri wa miaka 10, alichagua masomo ya mitindo. Akiwa na miaka 17, aligundua hakuwa sahihi katika uchaguzi, hivyo akabadili na kusomea ualimu.

UDHIBITI WA UTORO SHULENI

Katika kuhakikisha wanafunzi wanakwenda sawia na mifumo hiyo, Serikali ya Uholanzi imeweka utaratibu mzuri wa kudhibiti utoro shuleni.

Si tu kuacha shule, bali pia mwanafunzi kuchelewa darasani mara kwa mara ni suala linalopewa uzito mkubwa, ikiwamo maofisa wa mahudhurio ya wanafunzi katika Manispaa husika kupewa taarifa.

Utoro pasi husabaisha mzazi au mlezi kutozwa faini au mwanafunzi kupewa adhabu ya kufanya kazi za kijamii kwa lengo la kumrudisha kwenye mstari.

Wakati huo huo, Serikali imezitengea bajeti nzuri shule zote ili kuhakikisha zinaratibu programu mbalimbali, zikiwamo za ushauri wa kisaikolojia, kwa wanafunzi ili kupunguza au kuondosha kabisa tabia za utoro.

Kama hiyo haitoshi, Alexander Koppelle ni mmiliki wa Taasisi ya Mooi Jong, ambayo imejikita katika kuwafuatulia, kuwaibua na kuwapa fursa nyingine nje ya shule vijana walioshindwa kuendelea na masomo.

“Lengo ni kuhakikisha hakuna kijana anayeachwa na mfumo uliowekwa na kubaki mtaani akiwa hajui anapaswa kuwa wapi,” anasema Koppelle.

AJIRA HUANZIA DARASANI

Katika umri wa miaka 16 tu, wanafunzi, hasa waliochagua elimu ya ufundi, wanaweza kuwa tayari wanaingiza kipato kwa ajira za muda, huku wakiendelea na masomo.

Destiny ni miongoni mwa wanufaika baada ya kupata ajira katika moja ya saluni huku akiendelea na masomo yake ya urembo.

“Nilihamia Uholanzi nikitokea Bonaire baada ya kuona kule nafasi za ajira ni chache. Nilivutiwa na namna mfumo wa elimu wa Uholanzi unavyotoa fursa nyingi,” anasema.

Kwa mujibu wa Asja van der Helm, ambaye ni Mwalimu wa Sekondari mjini The Hague, Uholanzi inaangalia uhitaji wa soko, kisha kutengeneza mfumo wa elimu unaoandaa watu wa kuziba mapengo yaliyopo.

“Vijana wanaochagua ufundi wanachukuliwa kama hazina muhimu kwa Taifa,” anasema Mwalimu huyo wa Shule ya Sekondari mjini The Hague.

Mwalimu Der Helm anasema masomo ya ufundi, hasa umeme na ujenzi, yamekuwa kimbilio la vijana wengi kutokana na malipo mazuri yanayopatikana kwenye taaluma hizo.

Kupitia Shirika la Bima la Taifa, Serikali ya Uholanzi pia imekuwa ikisaidia vijana wasio na ajira kwa kuwapatia fedha za kujikimu, sambamba na kuwaunganisha wanaotafuta ajira na waajiri katika sekta binafsi.

Related articles

Recent articles