32 C
New York

Walitamba lakini walistaafu bila kutia mguu Kombe la Dunia

Published:

LONDON, Uingereza

KOMBE la Dunia ni michuano mikubwa zaidi katika mchezo wa soka, hivyo ni ndoto ya kila mchezaji kucheza mashindano hayo ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Hata hivyo, isivyo bahati, kuna wachezaji wakubwa waliowahi kutokea na kuwika katika ulimwengu wa soka lakini hawakucheza michuano hiyo hadi wanastaafu.

ABEDI PELE

Ni baba wa mastaa wa timu ya Taifa ya Ghana ‘The Cranes’, Jordan na Andre Ayew, ambao kwa nyakati tofauti wameshiriki Kombe la Dunia wakiwa na kikosi hicho.

Hata hivyo, Pele hakucheza michuano hiyo licha ya kutamba katika ulimwengu wa soka, ikiwamo kutwaa mara tatu tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika, kubeba ubingwa wa AFCON, na kuipa Marseille mawili ya Ligue 1 na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

GEORGE WEAH

Mwafrika pekee aliyewahi kutwaa tuzo kubwa ya Mchezaji Bora wa Mwaka ya Ballon d’Or lakini alistaafu mwaka 2003 akiwa hajawahi kucheza Kombe la Dunia.

Mwaka 2002, angeweza kushiriki lakini timu yaje ya Taifa ilikosa tiketi ya kwenda kwenye michuano hiyo baada ya kuzidiwa pointi moja tu na wapinzani wao, Nigeria.

IAN RUSH

Mfungaji bora wa muda wote wa klabu ya Liverpool. Alitwaa mataji matano ya Ligi Kuu ya England, mawili ya Ulaya, matatu ya FA na matano ya Kombe la Ligi (sasa EFL Cup).

Licha ya kuifungia mabao 28 katika mechi 73, timu yake ya Taifa ya Wales haikufuzu Kombe la Dunia wala fainali za EURO hadi Rush anastaafu.

ERIC CANTONA

Akiwa kwenye kiwango bora pale Manchester United, timu yake ya Taifa ya Ufaransa ilishindwa kufuzu Kombe la Dunia mwaka 1990 na 1994.

Alistaafu akiwa na umri wa miaka 30, wakati huo akiwa na mataji matano ya Ligi Kuu ya England ndani ya misimu sita tu aliyocheza Man United.

GEORGE BEST

Wakati Ireland ya Kaskazini inafuzu kwa mara ya kwanza mwaka 1958, Best alikuwa kijana mdogo wa umri wa miaka 12 tu.

Ilipofuzu kwa mara ya pili na ya tatu katika miaka ya 1980, tayari Best alishamaliza kuwika akiwa Man United ya Ligi Kuu ya England.

ALFREDO DI STEFANO

Mshambuliaji huyo aligombewa na klabu mbili za Real Madrid na Barcelona, kabla ya kuchagua kwenda Santiago Bernabeu mwaka 1953.

Aliipa Madrid mataji matano ya Ulaya, nane ya La Liga katika miaka ya 1950 na 1960. Aliiongoza Hispania kufuzu Kombe la Dunia mwaka 1962 lakini hakucheza hata mechi moja kutokana na majeraha.

Related articles

Recent articles