KYIV, Ukraine
RAIA huyo wa Ukraine kwa sasa ni tishio kwenye tasnia ya ngumi za uzito wa juu duniani na atapanda ulingoni kesho Mei 23, 2026 kuzichapa na Rico Verhoeven wa Uholanzi.
Ndiyo, pambano hilo litapigwa Misri na Usyk mwenye umri wa miaka 39 atatetea mkanda wake wa WBC.
KIBOKO YA WAINGEREZA
Tangu alipotwaa ubingwa wa michuano ya Olimpiki mwaka 2012, Usky amekuwa moto wa kuotea mbali, akiwapiga mara mbili kila mmoja mabondia watatu wakubwa wa Uingereza – Anthony Joshua, Tyson Fury na Daniel Dubois.
Pambano lake la mwisho ni la Julai, 2025, ambapo alimtandika Dubois na kwa sasa Usyk anashikilia mikanda mikubwa mitatu (WBA (Super), WBO na WBC.
Kwamba hajawahi kupigwa katika mapambano yake 24 ya ngumi za kulipwa, akishinda mara 15 kwa ‘KO’.
PAMBANO LILILOMPA HASIRA
Mara ya mwisho kupigwa lilikuwa ni pambano la ngumi za ridhaa (siyo za kulipwa) mwaka 2009, ambapo alitandikwa na Egor Mekhontsev wa Urusi.
Ni miaka 16 iliyopita. Ni kabla hata hajamuoa mke wake wa sasa, Yekatarina. Usky anasimulia namna pambano hilo lilivyompa hasira na kumjenga zaidi.
“Baada ya pambano hilo, nilirudi chumbani na kumuomba Mungu. Nilijisemea ‘sikia Olek, umepoteza pambano kwa sababu hukujituma vya kutosha ili kushinda. Unapaswa kufanya kazi ya ziada na kuacha kufanya makosa’,” anasimulia Usyk.
KUGEUKIA SOKO LA MUVI
Akiwa kwenye kambi ya maandalizi nchini Hispania, amefichua mipango yake ya baadaye akisema anataka kuwa mwigizaji wa filamu.
“Sitostaafu baada ya pambano hili (dhidi ya Rico). Labda nitakuwa na mapambano mengine mawili au matatu. Nina mpango wa kugeukia uigizaji. Nataka kufanya biashara hiyo …” amesema.


