Na Hassan Mwasha, Gazetini
KWA misimu mitano ya hivi karibuni, KMC imekuwa ikinusurika kwenye mtego wa kushuka daraja lakini huenda safari hii ikashindwa kujinasua na kurudi Championship (Ligi Daraja la Kwanza Bara).
Msimu huu umekuwa mbaya zaidi kwa timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni, ambapo imekusanya pointi tisa pekee katika mechi zake 23 za Ligi Kuu, ikishinda mechi mbili, sare tatu na kufungwa 18. Mabao ya kufungwa ni 39, idadi ambayo ni mara tatu ya iliyofunga (13).
Kwa mwenendo huo, hata ikishinda michezo yake saba iliyobaki, bado KMC itakwamia pointi 30, ambazo ni chache zaidi kuwahi kuzikusanya katika misimu mitano ya hivi karibuni.
Msimu uliopita, 2024-25, KMC waliumaliza wakiwa nafasi ya 10 kwenye msimamo lakini walikusanya pointi 35 tu baada ya kushuka dimbani mara 30. Katika mechi hizo, walishinda tisa pekee, sare nane na kufungwa 13.
2023-24, licha ya kushika nafasi ya tano kwenye msimamo, KMC ilimaliza msimu huo ikiwa na pointi 37 tu katika michezo 30. Ilishinda nane pekee, sare 13 na kufungwa tisa. Ilifunga mabao 27 na kuruhusu 39.
2022-23, KMC ilikusanya pointi 32 na kumaliza ikiwa nafasi ya 13 kwenye msimamo. Katika mechi 30, ilishinda nane, sare nane na kufungwa mara 14. Ilifunga mabao 25, pia ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 31.
2021-22, ni msimu ambao KMC ilimaliza ikiwa nafasi ya 10 kwenye msimamo, ikiwa na pointi 35 baada ya kucheza mechi 30. Ilishinda mechi nane pekee, sare 11 na kufungwa 11, ikifunga mabao 34 na kufungwa 35.


