12.1 C
New York

Mahakama yafufua hoja ya kumng’oa Ramaphosa

Published:

JOHANNESBURG, Afrika Kusini

RAIS wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, anakabiliwa na presha mpya ya kisiasa baada ya Mahakama ya Katiba kuamua kuwa Bunge lilikosea kisheria kwa kuzuia mchakato wa kumuondoa madarakani mwaka 2022.

Uamuzi huo umeibua upya mjadala mkubwa wa kisiasa nchini humo, huku kiongozi wa upinzani, Julius Malema, akimtaka Ramaphosa kujiuzulu mara moja.

Kesi hiyo ilifunguliwa na vyama vya upinzani, vikiwemo chama cha EFF kinachoongozwa na Malema, baada ya madai ya ukiukwaji wa sheria kufuatia sakata lililotikisa utawala wa Ramaphosa miaka mitatu iliyopita.

Chanzo cha mgogoro huo ni tukio la mwaka 2022 ambapo zaidi ya dola 500,000 ziliripotiwa kuibwa katika nyumba ya mashambani ya Ramaphosa. Kilichozua mjadala mkubwa ni madai kwamba fedha hizo zilikuwa zimefichwa ndani ya sofa, hali iliyowafanya wengi kuhoji chanzo na uhalali wa fedha hizo. Hata hivyo, Ramaphosa aliendelea kukanusha kufanya kosa lolote.

Wakati huo, chama tawala cha ANC kilikuwa na wabunge wengi bungeni, jambo lililosaidia kuzima juhudi za upinzani za kutaka kuanzishwa kwa mchakato wa kumuondoa rais madarakani.

Lakini mazingira ya kisiasa sasa yamebadilika. Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2024, ANC ilipoteza wingi wa moja kwa moja bungeni na kulazimika kuunda Serikali ya Muungano, hali inayoongeza uwezekano wa hoja mpya dhidi ya Ramaphosa kupata uungwaji mkono mkubwa.

Msemaji wa ANC, Mahlengi Bhengu, amesema chama hicho kinaheshimu uamuzi wa Mahakama ya Katiba na kwamba viongozi wa chama watakutana kujadili hatua zinazofuata.

Kwa upande wake, Malema amesema wakati umefika kwa Ramaphosa kuachia madaraka na kuruhusu mchakato wa uwajibikaji kufanyika wazi mbele ya sheria na wananchi.

Uamuzi huo wa Mahakama sasa unaonekana kufungua ukurasa mpya wa mvutano wa kisiasa nchini Afrika Kusini, huku macho ya wengi yakielekezwa bungeni kuona kama kweli safari ya Ramaphosa kuelekea kuondolewa madarakani inaweza kuanza upya.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img