4.3 C
New York

Unavyoweza kumkuza mtoto mwenye upendo na kujali wengine

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

MALEZI ya mtoto hayahusu chakula, mavazi au elimu pekee, bali pia maadili anayojifunza akiwa mdogo. Wazazi wengi hutamani kuona watoto wao wakikua wakiwa na upendo, huruma na uwezo wa kuwajali wengine. Mtoto anayejali hisia za watu na kuishi vizuri na jamii huwa rahisi kupendwa na kuheshimiwa.

Lakini swali muhimu ni hili: mzazi anawezaje kumlea mtoto mwenye tabia ya upendo na kujali wengine? Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa kuna mambo kadhaa muhimu yanayoweza kusaidia.

Watoto hujifunza zaidi kwa kuona kuliko kusikia. Hivyo, mzazi anapaswa kuonyesha mfano wa utu na heshima kwa watu wengine. Watendee watu kwa wema na heshima bila kujali hadhi au nafasi yao katika jamii. Hata unapokuwa na tofauti za maoni na wengine, onyesha jinsi ya kutofautiana kwa ustaarabu.

Unapokutana na mtu anayefanya jambo la kiungwana kwa wengine, eleza hilo kwa mtoto wako na umwambie kwa nini limekugusa. Kwa kuwa wewe ndiye mwalimu wa kwanza wa mtoto wako, maneno na matendo yako yana nguvu kubwa katika kumjenga.

Jiulize pia: unaongeaje na majirani wasio na uwezo kama wewe? Unamzungumziaje mlinzi wa geti lako au mfanyakazi wa nyumbani? Unaishi vipi na ndugu zako kama shemeji au mawifi? Watoto huwa makini sana kuchunguza matendo ya wazazi wao, na mara nyingi huiga kile wanachokiona.

Ni muhimu kuwafundisha watoto kuwa maisha siyo kujitafutia tu mahitaji binafsi. Wazazi wanapaswa kuwahamasisha watoto kushiriki katika matendo ya kusaidia wengine, kutoa na kujitolea.

Kwa mfano, kama una nguo au viatu ambavyo havitumiki tena, unaweza kuwapa watu wenye uhitaji. Mtoto akiona unafanya hivyo, anajifunza kuwa kuwasaidia wengine ni jambo la kawaida na la thamani.

Pia unaweza kutenga muda kwenda kanisani au msikitini kufanya usafi pamoja na watoto, au kutembelea vituo vinavyowahudumia watu wenye mahitaji maalum na kuwasaidia kwa kadiri ya uwezo wako. Matendo kama haya hupanda mbegu ya huruma na ukarimu moyoni mwa mtoto.

Wazazi wengi huzungumzia umuhimu wa upendo, lakini wakati mwingine hawaonyeshi kwa vitendo. Watoto wanapoambiwa wasamehe wengine lakini wakawaona wazazi wao hawasamehi, hupata ujumbe unaochanganya.

Ili mtoto ajifunze kuwajali wengine, anza kwa kumjali yeye. Mwonyeshe huruma pale anapokosea na usiwe na tabia ya kuweka visasi. Msamehe na umwelekeze kwa upendo.

Kila tendo la upendo unalofanya mbele ya mtoto wako ni somo muhimu kwake. Mtoto anayekulia katika mazingira ya upendo hushiba hisia hizo na baadaye ana uwezo wa kuwasambazia wengine.

Kinyume chake, mtoto asiyepata uhakika wa kupendwa anaweza kukua akiwa na njaa ya upendo, hali inayoweza kumfanya awe na chuki au ugumu wa kuhusiana vizuri na wengine. Uhusiano wa mzazi na mtoto ndio unaoweka msingi wa mahusiano yake na watu wengine maishani.

Hatimaye, ili mtoto aweze kuwapenda wengine, lazima ajifunze kujipenda. Hata hivyo, kujipenda huanzia kwa mzazi. Unapaswa kuonyesha kuwa unathamini maisha yako na unafurahia ulivyo.

Ni vigumu kushughulikia mahitaji ya mtoto ikiwa mzazi mwenyewe anaishi katika hali ya hasira au msongo wa mawazo. Huwezi kuwajali wengine kama hujijali mwenyewe.

Aidha, watoto hujifunza upendo kwa kuwaona wazazi wao wakiheshimiana na kupendana. Upendo kwa watoto mara nyingi huanzia katika upendo uliopo kati ya wazazi wao. Wazazi wanapoishi kwa upendo na heshima, wanawawekea watoto wao msingi imara wa kuwa watu wenye huruma, heshima na upendo kwa wengine.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img