8.4 C
New York

Ndejembi: Haki za wafanyakazi zinapaswa kusimamiwa ipasavyo

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

WAZIRI wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amefungua Kikao cha 55 cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kinachofanyika mkoani Dodoma, akisisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti wa haki za wafanyakazi na uboreshaji wa huduma za umeme nchini.

Akizungumza leo Januari 22, 2026, wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Ndejembi alimpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuboresha maslahi na stahiki za wafanyakazi wa TANESCO, hatua aliyosema imeongeza ari na ufanisi kazini.

“Ninamshukuru Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha maslahi na stahiki za wafanyakazi wa TANESCO. Hili limechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza morali na uwajibikaji katika utendaji wa shirika,” alisema Waziri Ndejembi.

Alisisitiza kuwa haki za wafanyakazi zinapaswa kusimamiwa ipasavyo kwa kuimarisha ushirikiano mahali pa kazi, pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu huduma ya umeme.

“Natambua mmekutana hapa kujadili kwa kina masuala yanayowahusu wafanyakazi. Naomba mhakikishe mnazungumza kwa uwazi na kukubaliana kwa pamoja ili kuendelea kuboresha utendaji wa shirika na maslahi ya wafanyakazi,” aliongeza.

Aidha, Waziri Ndejembi aliwahimiza viongozi na wafanyakazi wa TANESCO kuendelea kuboresha utoaji wa huduma bora na za uhakika za umeme kwa wananchi, akibainisha kuwa upatikanaji wa umeme wa kuaminika ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, alimshukuru Waziri Ndejembi kwa kukubali wito wa kufungua kikao hicho na kumuahidi kuwa uongozi wa shirika utaendelea kusimamia haki za wafanyakazi na kuhakikisha maamuzi yanayotolewa yanatekelezwa kwa vitendo.

“Kipekee nikushukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuitikia wito wa kuja kutufungulia kikao hiki. Kama Mwenyekiti wa Baraza hili, nikuahidi kuwa nitasimamia kikamilifu yote yatakayojadiliwa hapa kwa lengo la kuleta tija, maendeleo ya TANESCO na kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi,” amesema Twange.

Kikao hicho cha siku kadhaa kimewakutanisha viongozi wa TANESCO, wawakilishi wa Chama cha Wafanyakazi (TUICO), Wakurugenzi wa Kanda, pamoja na wawakilishi wa wafanyakazi kutoka kampuni tanzu na ofisi mbalimbali za mikoa nchini, ambapo wanajadili masuala ya ustawi wa wafanyakazi, mazingira ya kazi na ufanisi wa shirika.

 

 

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img