9.8 C
New York

Japan kuvunja bunge, kusimamisha kodi ya chakula kwa miaka miwili

Published:

TOKYO, Japan

WAZIRI Mkuu wa Japan, Sanae Takaichi, Jumatatu ametangaza kuitisha uchaguzi mkuu wa ghafla, akiahidi kusimamisha kwa miaka miwili ushuru wa matumizi wa asilimia 8 unaotozwa kwa vyakula, hatua inayolenga kupunguza mzigo wa gharama ya maisha kwa kaya, lakini ambayo imeibua wasiwasi kuhusu mustakabali wa kifedha wa taifa hilo.

Ahadi hiyo inafanana na mapendekezo yaliyotolewa na vyama vya upinzani, hata hivyo wachambuzi wanaonya kuwa kupunguza kodi hiyo kunaweza kuacha pengo kubwa katika mapato ya serikali, wakati ambao tayari Japan inakabiliwa na hali tete ya kifedha na kuongezeka kwa riba ya hati fungani (bond yields) hadi viwango vya juu zaidi kwa miongo kadhaa.

Kwa sasa, Japan inatoza ushuru wa matumizi wa asilimia 8 kwa vyakula na asilimia 10 kwa bidhaa na huduma nyingine, mapato yanayotumika kugharamia ongezeko la matumizi ya ustawi wa jamii katika nchi yenye idadi kubwa ya wazee. Takaichi amesema kusimamishwa kwa kodi ya chakula kwa miaka miwili kutasaidia kaya kukabiliana na kupanda kwa gharama za maisha, akisisitiza kuwa serikali haitakopa fedha kufadhili hatua hiyo, bali itapitia upya ruzuku zilizopo na hatua nyingine za kifedha.

“Tutafanya mageuzi ya sera za zamani za uchumi na fedha. Serikali yangu itasitisha sera kali za kubana matumizi na upungufu wa uwekezaji kwa ajili ya baadaye,” Takaichi alisema katika mkutano na waandishi wa habari.

Tangazo la uchaguzi na matarajio ya kupunguzwa kwa kodi ya matumizi yamesababisha riba ya hati fungani ya serikali ya Japan ya miaka 10 kupanda hadi asilimia 2.275, kiwango cha juu zaidi katika kipindi cha miaka 27, huku masoko yakitarajia ushindi wa Takaichi kuimarisha sera zake za upanuzi wa matumizi ya serikali. Hata hivyo, wachumi wameonya dhidi ya athari zake.

Wakati huo huo, vyama vya upinzani vimekuwa vikitoa wito wa kupunguzwa au kuondolewa kabisa kwa kodi ya matumizi kuelekea uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Februari 8, vikirejea malalamiko ya wananchi kuhusu mfumuko wa bei. Chama kipya cha kisiasa kilichoundwa wiki iliyopita kutokana na muungano wa vyama viwili vikuu vya upinzani kimependekeza kufutwa kabisa kwa ushuru wa asilimia 8 kwa vyakula, kikisema Japan inaweza kuanzisha mfuko wa uwekezaji wa taifa (sovereign wealth fund) kufidia mapato yatakayopotea.

Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa kuondoa ushuru wa chakula wa asilimia 8 kungepunguza mapato ya serikali kwa takribani trilioni 5 za yen kwa mwaka (sawa na dola bilioni 31.7), kiasi kinachokaribiana na bajeti ya kila mwaka ya sekta ya elimu. Wachambuzi wanaonya kuwa kupunguza kodi hiyo kwa kudumu kunaweza kuongeza presha kwa fedha za serikali na kuchochea uuzaji wa hati fungani, hasa ikizingatiwa kuwa serikali ya Takaichi tayari imeandaa bajeti ya rekodi ya dola bilioni 783 kwa mwaka ujao wa fedha, sambamba na mfuko mkubwa wa kichocheo cha uchumi kupunguza athari za gharama ya maisha.

Chama tawala cha Liberal Democratic Party (LDP) kwa muda mrefu kimekuwa kikikataa wito wa kupunguza kodi ya matumizi, kikisema hatua hiyo inaweza kudhoofisha imani ya masoko katika dhamira ya Japan ya kurekebisha hali yake ya kifedha. Hata hivyo, kwa mfumuko wa bei uliovuka lengo la Benki Kuu ya Japan la asilimia 2 kwa karibu miaka minne mfululizo, shinikizo la kisiasa la kupunguza kodi na kuongeza matumizi linaendelea kuongezeka.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img