Na mwandishi wetu, Gazetini
KUTOKA maisha ya ‘kuungaunga’ katika makazi ya watu wa kipato cha chini mjini Kampala, na sasa ni mwanasiasa maarufu na anayempa wakati mgumu Rais Yoweri Museveni, ambaye amekuwa Ikulu kwa miaka 40.
Anaitwa Bobi Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi Ssentamu. Alizaliwa mwaka 1982 mjini Kampala.
Akibebwa zaidi na umri na historia ya kutokea familia ya kimasikini, siasa za Uganda zinamchora kama tumaini la vijana wenye kiu ya kuona mabadiliko makubwa ya kiuchumi nchini humo.
Si tu wanataka mapinduzi ya kiuchumi, vijana ambao ni asilimia 70 ya raia wa Uganda, bali pia wanaamini viongozi wa umri wa Museveni (miaka 81) hawana jipya.

Na badala yake, wanaamini kuwa vijana kama Bobi Wine (43) wanapaswa kupewa nafasi ya kuongoza ili kuleta fikra mpya zinazoendana na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia duniani.
Kupitia mwamvuli wa Chama cha National Unity Platform (NUP), Bobi Wine amejidhatiti kumkabili Rais Museveni katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika siku chache zijazo (Januari 15, 2026).
Kama ilivyokuwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2021, ambapo Bobi Wine alimkaba koo Rais Museveni aliyepata ushindi kiduchu wa asilimia 58.6 ya kura, safari hii Bobi Wine bado ana ushawishi mkubwa.
Bobi Wine amejikusanyia ‘kijiji’ cha vijana, wengi wao wakiamini ni wakati wa Rais Museveni kupumzika na kumpisha kijana mwenzao kushika nafasi hiyo nyeti.
Hata hivyo, kizingiti kikubwa kilicho mbele yake ni namna Rais Museveni anavyotumia vyombo vya dola kumdhibiti, kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa za Ukanda wa Afrika Mashariki.
Kuelekea Uchaguzi wa mwaka 2021, Bobi Wine alikamatwa mara zaidi ya 30, ikiwamo kutokuonekana kwa siku 12 mwanzoni mwa mwaka 2020.
Wakati huo, itabaki kwenye historia kuwa Bobi Wine alikumbana na mateso makali akiwa kizuizini, ikiwa ni pamoja na kupigwa risasi mguuni.
Nje ya hapo, mikutano yake ya kampeni ilivamiwa mara kadhaa na vyombo vya dola, pia akizuiwa kufanya matamasha ya muziki kwa kile mamlaka ilichodai kuwa ni kujikinga na vurugu.
Vurugu zilizohusiana na Uchaguzi zilisababisha vifo vya watu zaidi ya 50, wengi wao wakiwa ni wafuasi wa Bobi Wine.
Kupitia ripoti yake, Tume ya Haki za Binadamu ya Uganda iliweka wazi kuwa mazingira kabla ya Uchaguzi hayakuruhusu upatikaji wa haki.
Tume ilitolea mfano kufungwa kwa huduma ya mtandao kwa siku tano na kusababisha kukosekana kwa uhuru wa kupashana habari, hasa zinazohusu Uchaguzi.
Kwa upande wake, Bobi Wine naye alijaribu kupinga matokeo ya Uchaguzi kwa kulifikisha suala hilo Mahakama Kuu, ambayo hata hivyo haikumzuia Rais Museveni kuapishwa Mei 12, 2021.
Kama itakumbukwa, polisi walizingira nyumba ya Bobi Wine kwa wiki kadhaa, kabla ya mwanasiasa huyo kufungwa kifungo cha ndani.
Tangu hapo, Bobi Wine ameendelea kujenga misingi imara ya Chama chake cha NUP. Mathalan, kuteua baadhi ya wasanii kugombea ubunge ni hatua nzuri ya kuvuna ushawishi zaidi, hasa kwa kundi la vijana.
Pia, baada ya kile kilichotokea katika Uchaguzi wa mwaka 2021, Bobi Wine amefanikiwa kukitangaza NUP nje ya mipaka ya Uganda, ikiwamo ziara yake katika Chuo Kikuu cha Ulaya mwaka 2024.
Kupitia ziara hiyo, aliweza kukutana na kuzungumza na wadau mbalimbali wa sera, demokrasia na haki za binadamu.
Je, jitihada hizo, pamoja na nguvu ya vijana, vitamwezesha Bobi Wine kumpiku Rais Museveni ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1986? Ni suala la kusubiri na kuona.


