CARACAS, Venezuela
DELCY Rodríguez ameapishwa kuwa rais wa mpito wa Venezuela katika kikao cha Bunge kilichoanza kwa wito wa kumwachilia huru rais aliyeondolewa madarakani na kuzuiliwa nchini Marekani, Nicolás Maduro.
Rodríguez (56), ambaye amekuwa makamu wa rais tangu mwaka 2018, amesema amesikitishwa na kile alichokitaja kuwa ni “utekaji nyara” wa Maduro na mkewe, Cilia Flores, waliokamatwa na vikosi vya Marekani katika operesheni ya usiku wa kuamkia Jumamosi.

Huku hayo yakijiri Caracas, matukio ya kushangaza yalishuhudiwa ndani ya chumba cha mahakama jijini New York saa kadhaa kabla, ambapo Maduro alisisitiza kuwa bado ndiye rais halali wa Venezuela, akikana mashtaka manne yanayomkabili ya ulanguzi wa dawa za kulevya na ugaidi.
Hatua ya Marekani imekosolewa vikali katika Umoja wa Mataifa, huku baadhi ya nchi zikieleza wasiwasi kuhusu ukiukwaji wa sheria za kimataifa. Hata hivyo, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amesema hifadhi kubwa zaidi ya nishati duniani haiwezi kuachwa mikononi mwa kiongozi aliyemtaja kuwa ni haramu na “mkwepaji wa haki”.
Kabla ya Maduro kufikishwa mahakamani, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilifanya kikao cha dharura kujadili hali ya kisiasa na kiusalama nchini Venezuela.
Balozi wa Venezuela katika Umoja wa Mataifa, Samuel Moncada, amesema nchi yake imelengwa na “shambulio haramu la kijeshi lisilo na uhalali wowote wa kisheria”.
Kwa upande wake, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Mike Waltz, alitetea operesheni hiyo kwa kumtaja Nicolás Maduro kama “rais haramu” asiye na uhalali wa kuendelea kuongoza taifa hilo.


