Na mwandishi wetu, Gazetini
LICHA ya mataifa mengi duniani kutambua na Serikali zake kuendeshwa kwa misingi ya demokrasia, yapo baadhi yasiyotambua utaratibu huo.
Kwa takwimu za sasa, kwa mujibu wa mtandao wa World Visualized, mataifa hayo ni Afghanistan, Brunei, Oman, Qatar, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Vatican.
Brunei ni nchi ya kisultani, ikiongozwa na Sultani Hassanal Bolkiah, ambaye ndiye anayehodhi majukumu ya Waziri Mkuu, Waziri wa Ulinzi na Waziri wa Fedha nchini humo.
Mara ya mwisho kwa Taifa hilo kufanya Uchaguzi wa wabunge ilikuwa mwaka 1962. Baraza maalumu, ambalo wajumbe wake huteuliwa na Sultan, ndiyo washauri wa Serikali.
Vatican, kwa upande wake, kiongozi anayekuwa kama Rais, ni Papa, ambaye ndiye anayemsimamia utendaji wa Bunge, Mahakama na Serikali kwa ujumla.
Kwa upande wa Saudi Arabia, Oman, Qatar na UAE, uongozi ni wa kifalme, ambao hurithishwa kutoka kizazi kimoja na kingine.
Ni katika muundo wake, familia ya kifalme ndiyo yenye nguvu na ushawishi mkubwa katika kuiongoza Serikali, licha ya kwamba ipo Bodi ya ushauri.


