Na mwandishi wetu, Gazetini
KUMEKUCHA! Droo ya hatua ya makundi ya fainali za Kombe la Dunia ilichezeshwa nchini Marekani.
Kwa mara ya kwanza, fainali hizo zitashirikisha mataifa 48, huku mechi 104 zikitarajiwa kuchezwa katika viwanja mbalimbali vya Marekani, Mexico na Canada.
Tukijikumbushe; timu 42 zilishakata tiketi na sasa zinasubiriwa zingine sita zitakazopatikana kupitia mechi za ‘play-off’ zitakazochezwa Machi, mwakani.
Sasa, makala haya yanaliangazia Kundi H na kuchambua timu zilizopo kuelekea michuano hiyo itakayoanza Juni 11, mwakani.
Kundi hili linazikutanisha Hispania, Cape Verde, Saudi Arabia na Uruguay. Mabingwa wa Ulaya, Hispania, wanashika nafasi ya kwanza katika viwango vya ubora wa soka duniani.
Katika mechi zao za kuwania tiketi, walidondosha pointi mbili pekee, pia wakiwa na wastani wa kufunga mabao matatu kila waliposhuka dimbani.
Vigogo wa soka la Kusini mwa Amerika, Uruguay, wao wanateswa na ‘mzimu’ wa matokeo mbaya, ikiwamo kufungwa mabao 5-1 na Marekani mwezi uliopita.
Cape Verde, kwa upande wao, walianza kuwika katika soka la Afrika mwaka 2013, baada ya kushiriki kwa mara ya kwanza fainali za AFCON.
Safari hii, wako Kombe la Dunia, ingawa wameikosa tiketi ya kushiriki fainali hizo za Mataifa ya Afrika.
Kwa upande wa Saudi Arabia, wamemrejesha kwenye benchi la ufundi kocha wao wa zamani raia wa Ufaransa, Herve Renard. Je, watakuwa na jipya hapo mwakani?


