WASHINGTON DC, Marekani
RAIS wa Marekani, Donald Trump, ameendelea kumpa presha mwenzake wa Venezuela, Nicolas Maduro.
Hivi karibuni, utawala wa Trump ulitangaza kuongeza mara mbili zawadi ya fedha kwa atakayefanikisha kukamatwa kwa Rais huyo wa Venezuela.
Hatua hiyo imeenda sambamba na mshambulizi kwa meli za Venezuela kwa madai kuwa zinasafirisha dawa za kulevya kuingiza Marekani. Imeripotiwa pia, kwamba Rais Trump alizungumza kwa simu na Maduro mwezi uliopita na kumtaka kiongozi huyo kuondoka Vanezuela.
Historia inaonesha kuwa katika safari yake ya maisha, Maduro aliwahi kuwa dereva wa basi, kabla ya kuingia kwenye siasa na hatimaye kuingia madarakani mwaka 2013.
Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, 2024, Maduro alirejea madarakani, ingawa matokeo ya ushindi yalipingwa kwa taarifa kuwa mpinzani wake, Edmundo Gonzalez, ndiye aliyestahili kuingia Ikulu.
Marekani na washirika wake zilitangaza ushindi wa Maduro kuwa ni batili na kusema zinamtambua Gonzalez kuwa ndiye rais anayetakiwa na wananchi wa Venezuela. Hata hivyo, kutokana na nguvu kubwa aliyonayo Maduro mbele ya jeshi, polisi na Mahakama, Gonzalez alilazimika kukimbilia uhamishoni akihofia kukamatwa.
Tangu aliporejea madarakani, Rais Trump amekuwa akimlaumu Maduro akisema Marekani imekuwa ikipokea idadi kubwa ya wahamiaji wanaotoka Venezuela.
Kuanzia mwaka 2013, raia wa Vanezuela takribani milioni nane wamekimbilia Marekani kutokana na hali mbaya ya uchumi na siasa nchini kwao. Licha ya kukosa ushahidi, Rais Trump anamshutumu Maduro akidai amekuwa akiwalazimisha wafungwa kuondoka Venezuela na kwenda Marekani.
Wakati huo huo, utawala wa Rais Trump unaishutumu Venezuela kwa madai ya kuingiza dawa za kulevya aina ya cocaine nchini Marekani. Katika hilo, Marekani inayataja makundi mawili ya Venezuela, Tren de Aragua na Cartel de los Soles, na kuyaita ‘magaidi wa dunia wanaoongozwa na Maduro’.
Maduro, kwa upande wake, si tu amekana kuhusika, pia anasema Marekani inataka kutumia mwanya huo kuingia Venezuela na kuchota utajiri wa mafuta. Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya usalama wanasema hakuna kundi linaloitwa Cartel de los Soles, bali jina hilo wamepachikwa viongozi wa Serikali ya Venezuela wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Pia, wachambuzi wanasema Venezuela ni sehemu ndogo tu ya mtandao wa dawa za kulevya, tofauti na inavyoelezwa na Marekani.
Kwamba Venezuela sio mzalishaji, ingawa imekuwa ikitumika kama njia ya kusafirisha cocaine na aina zingine za dawa za kulevya.
Na badala yake, wachambuzi wanaitaja Colombia kuwa ndiyo mzalishaji mkubwa duniani lakini haiitumii Venezuela kama njia ya kusafirisha ‘unga’.
Hata ripoti ya mwaka 2020 ya Taasi ya Kupambana na Dawa za Kulevya ya Marekani inaonesha kuwa kiwango kikubwa kinachoingia nchini humo hakitokei Venezuela.
Mathalan, dawa za kulevya aina ya fentanyl huzalishwa zaidi Mexico na husafirishwa kwa njia ya ardhi, pia huingia Marekani kupitia mpaka wake wa Kusini.


