COPENHAGEN, Denmark
SHIRIKA la ujasusi la Denmark [PET] limelishutumu Urusi likiitaja kuhusika katika jaribio lililoshindikana la kumuua mwanamuziki wa Hip hop raia wa Marekani mwenye asili ya Ukraine.
Denmark imedai kuwa Urusi iliratibu mpango wa kumuua rapa huyo lakini jaribio hilo halikufanikiwa.
Albert Vasiliev, maarufu kwa jina la Kyivstoner, anatajwa kunusurika kifo Septemba, 2026, wakati alipokuwa kwenye shoo yake jirani na Mji Mkuu wa Copenhagen.
Kwa mujibu wa PET, mauaji hayo yalipangwa kufanikishwa na raia wa Denmark kwa kushirikiana na majasusi wa Urusi.
PET wameeleza kuwa walishirikiana na polisi kuwafuatilia watu watatu waliokuwa kwenye gari wakielekea kwenye shoo ya msanii huyo na ndipo walipobaini kuwa walikuwa na bastola na visu.
Hata hivyo, Ofisi ya ubalozi wa Urusi nchini Denmark imekanusha taarifa hiyo na kusisitiza kuwa madai hayo yamekosa ushahidi.
Wakati huo huo, mamlaka za Denmark zimeeleza kuwa Urusi ilijaribu kushirikiana na genge maarufu la wahuni la ‘Loyal to Familia’ kumuua mwanamuziki huyo.


