Na Hassan Mwasha, Gazetini – DAR
HUKUMU ya Novemba 6, 2026, ni kama imefuta kabisa matumaini na matarajio makubwa ya kutokea kwa kile kilichoitwa ‘maridhiano’ kati ya Serikali na Chama Kikuu cha upinzani hapa nchini, CHADEMA.
Kabla ya Tundu Lissu kuhukumiwa kifungo cha miaka minne gerezani kwa kosa la uchochezi, japo haikuwa kesi aliyoshitakiwa nayo, wengi walitarajia kuona ukurasa mpya ukiandikwa.
Labda matarajio ya wengi yalikuwa ni kumuona Mwenyekiti huyo wa CHADEMA akiachiwa huru ili kutoa nafasi kwa meza ya mazungumzo ya kusaka maridhiano ya pande mbili hizo [CHADEMA na Serikali].
Sasa, baada ya kile kilichotokea, ni wazi hakuna tena uwezekano wa maridhiano au yatachukua muda mwingine mrefu kutokea. Na kama yatatokea kipindi hiki, basi ni nje ya ushiriki wa CHADEMA.
Ndiyo, ni rahisi kubashiri kuwa viongozi wa CHADEMA walioko uraiani hawatokuwa tayari kukaa mezani na upande wowote unaoitisha maridhiano wakati huu mwenzao akisota kwenye kuta za gereza.
Hatari ya kukubali ‘mwaliko’ ni kwamba watatafsiriwa kuwa ni wasaliti na inaweza kuwa hatua ya kwanza ya mwisho wa ushawishi mkubwa ilionao CHADEMA mbele ya wananchi wanaokiunga mkono Chama hicho.
Pia, endapo itatokea yakafanyika mazungumzo pasi na ushiriki wa CHADEMA, kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia vyama vingine vya siasa vikiitwa mezani, basi maridhiano hayo yatakosa mantiki.
Kwanini? Kama ilivyowahi kutokea kwa NCCR-Mageuzi na CUF miaka mingi iliyopita, CHADEMA kwa sasa ndiyo nembo halisi ya ushindani wa siasa za upinzani hapa nchini. Wanaoitakia mema demokrasia ya nchi hii hawawezi kukipuuza.
Mathalan, leo hii tunavyozungumzia mkwamo wa kisiasa uliopo, si kwa sababu ya CUF, ACT-Wazalendo, CHAUMMA au NCCR-Mageuzi. CHADEMA ndiyo ‘sterling’ wa filamu hiyo ya ‘mkwamo wa kisiasa’.
Kwanini? Hebu tutafakari na kujiuliza; endapo CHAUMMA kingesusia Uchaguzi uliopita wa Mwaka 2025, kama ilivyofanya CHADEMA, nani leo hii angezungumzia maridhiano?
Hivyo, kwa Chama chenye ushawishi mkubwa kama CHADEMA, litakuwa ni jambo la kustaajabisha mno na lisilo na afya kwa ustawi wa demokrasia kuona kikikosa nafasi kwenye meza ya maridhiano ya kitaifa.
Ni kwa maana hiyo basi, Lissu ndiye aliyeshika funguo za unaoweza kuitwa ‘mlango wa kuingia kwenye maridhiano’. Ni aidha atoke gerezani na kufungua mlango huo, abaki na funguo zake huko aliko.
Kinyume cha hayo yote, maridhiano yatakayofanyika nje wakati Lissu akiwa hajatoka gerezani hayatotofautiana na tukio la kulazimisha kuingia ndani kwa kuvunja mlango baada ya kukosa ufunguo.


