10.5 C
New York

Mtoto wa kishua anayeitikisa dunia, wazazi walimtupa…

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

DONALD John Trump ni miongoni mwa marais wenye ushawishi na utata mkubwa katika historia ya kisiasa ya Marekani. Kauli zake, maamuzi na mtindo wake wa uongozi vimeendelea kuvuta mijadala ndani na nje ya nchi hiyo, tangu alipoingia Ikulu kwa mara ya kwanza mwaka 2017 hadi kurejea madarakani mwaka 2025.

Safari yake haikuanza katika siasa, bali katika familia tajiri ya wafanyabiashara wa majengo jijini New York, ambako alikulia akizungukwa na maisha ya utajiri na fursa za kibiashara.

Trump alizaliwa Juni 14, 1946, katika eneo la Queens, New York, akiwa mtoto wa nne kati ya watoto watano wa Fred Trump na Mary Anne MacLeod Trump.

Baba yake, Fred, alikuwa mfanyabiashara maarufu wa ujenzi na upangishaji wa majengo, aliyekuwa na kampuni iliyojihusisha zaidi na ujenzi wa nyumba na makazi ya watu wenye kipato cha kati katika maeneo ya New York.

Licha ya kukulia katika familia yenye uwezo mkubwa kifedha, Trump hakupita bila changamoto katika malezi yake. Akiwa na umri wa miaka 13, wazazi wake walimpeleka katika Chuo cha Kijeshi cha New York (New York Military Academy), wakitarajia nidhamu ya kijeshi ingemsaidia kurekebisha tabia zake za utotoni.

Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Fordham kabla ya kuhamia Chuo Kikuu cha Pennsylvania, ambako alihitimu Shahada ya Uchumi kupitia Shule ya Biashara ya Wharton mwaka 1968.

ALIVYOJENGA HIMAYA YA BIASHARA

Baada ya kuhitimu, Trump alijiunga kikamilifu na biashara ya familia iliyokuwa ikiendeshwa na baba yake. Mwaka 1971, alichukua usimamizi wa kampuni hiyo na baadaye kuipa jina la Trump Organization.

Awali biashara hiyo ilijikita katika ujenzi na upangishaji wa majengo ya makazi, lakini Trump alikuja kuipanua na kuingia katika maeneo mengine ya uwekezaji.

Alielekeza nguvu zake katika soko la majengo ya kifahari jijini Manhattan, New York, huku akipanua uwekezaji katika hoteli, kasino, viwanja vya gofu na maeneo ya mapumziko ndani na nje ya Marekani.

Miongoni mwa mambo yaliyompa umaarufu katika biashara ni uwezo wa kutumia jina lake kama chapa ya kibiashara, ambapo jina Trump lilianza kuonekana katika majengo, hoteli na bidhaa mbalimbali.

Safari hiyo ya biashara haikuwa bila misukosuko. Baadhi ya kampuni zake za kasino na hoteli zilikumbwa na matatizo ya kifedha na kufikia hatua ya kuomba ulinzi wa kisheria dhidi ya wadai kupitia utaratibu wa kufilisika kwa kampuni. Hata hivyo, aliendelea kujijenga kama mfanyabiashara maarufu nchini Marekani.

Mwaka 1987 alichapisha kitabu chake The Art of the Deal, kilichoelezea falsafa yake ya kufanya biashara na namna alivyokuwa akijenga mikataba mikubwa. Kitabu hicho kilimsaidia kuongeza umaarufu wake nje ya sekta ya biashara.

Umaarufu wake uliendelea kukua mwaka 2004 alipoanza kuongoza kipindi cha televisheni cha The Apprentice, ambacho kilimfanya ajulikane zaidi kwa watazamaji wa Marekani na kimataifa.

Katika kipindi hicho, alijenga taswira ya mfanyabiashara mwenye mamlaka ya kufanya maamuzi magumu, huku kauli yake maarufu ya kumwondoa mshiriki aliyeshindwa katika changamoto za biashara ikimpa umaarufu zaidi.

SIASA ZILIVYOMVUTA

Ingawa kwa muda mrefu Trump alijitambulisha zaidi kama mfanyabiashara, wazo la kuwania urais halikuwa geni kwake.

Mwaka 1987 alianza kuonesha nia ya kuingia katika siasa za urais, lakini hakuwahi kuwasilisha kampeni rasmi ya kuwania nafasi hiyo wakati huo.

Hatimaye, Juni 16, 2015, alitangaza rasmi kugombea urais kupitia Chama cha Republican, akitumia kaulimbiu ya Make America Great Again, yenye maana ya kuifanya Marekani kuwa kubwa tena.

Kampeni yake ilijikita katika ahadi za kuimarisha uchumi, kupunguza uhamiaji usio halali, kurekebisha mikataba ya biashara na kuweka maslahi ya Marekani mbele.

Licha ya kutokuwa na uzoefu wa kushika nafasi ya kuchaguliwa katika Serikali, Trump aliweza kuwashinda wapinzani wake ndani ya Chama cha Republican na kupata nafasi ya kuwania urais dhidi ya Hillary Clinton wa Chama cha Democratic.

Katika uchaguzi uliofanyika Novemba 8, 2016, Trump alimshinda Clinton katika kura za wajumbe wa majimbo (Electoral College), licha ya mpinzani wake kupata kura nyingi zaidi za wananchi kwa ujumla.

Januari 20, 2017, aliapishwa kuwa Rais wa 45 wa Marekani, akianza kipindi cha kwanza cha uongozi kilichodumu hadi Januari 20, 2021.

Katika uchaguzi wa mwaka 2020, alishindwa na Joe Biden na kuondoka madarakani, lakini hakujiondoa katika siasa. Aliendelea kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya Chama cha Republican na baadaye kutangaza tena kugombea urais.

Mwaka 2024 alishinda uchaguzi dhidi ya Kamala Harris, na Januari 20, 2025, akaapishwa kwa mara nyingine kuwa Rais wa Marekani.

Kurejea kwake madarakani kulimfanya kuwa rais wa 47 wa nchi hiyo na wa pili katika historia ya Marekani kuhudumu vipindi viwili visivyofuatana, baada ya Grover Cleveland.

MAISHA YA NDOA NA FAMILIA

Nje ya biashara na siasa, maisha ya ndoa ya Trump yamekuwa sehemu nyingine inayovuta hisia za umma kutokana na kuoa wanawake watatu na kupata watoto watano.

Ndoa yake ya kwanza ilikuwa na Ivana Zelnickova, mwanamitindo aliyezaliwa nchini Czechoslovakia, waliofunga ndoa mwaka 1977.

Katika ndoa hiyo walipata watoto watatu ambao ni Donald Trump Jr., Ivanka Trump na Eric Trump. Hata hivyo, ndoa yao ilivunjika mwaka 1992 baada ya miaka kadhaa ya kuwa pamoja.

Baada ya kuvunjika kwa ndoa hiyo, Trump alimuoa mwigizaji Marla Maples mwaka 1993. Kabla ya kufunga ndoa walikuwa tayari wamepata mtoto mmoja, Tiffany Trump, aliyezaliwa Oktoba mwaka huohuo.

Ndoa yao haikudumu kwa muda mrefu, kwani walitengana mwaka 1997 na talaka kukamilika mwaka 1999.

Baadaye, Trump alikutana na Melania Knauss, mwanamitindo aliyezaliwa nchini Slovenia, ambaye alimuoa Januari 22, 2005.

Katika ndoa hiyo walipata mtoto mmoja, Barron William Trump, aliyezaliwa Machi 20, 2006.

Melania amekuwa sehemu ya maisha ya kisiasa ya Trump, akihudumu kama Mke wa Rais katika vipindi vyake vyote viwili vya uongozi.

Kwa sasa Trump ana watoto watano, wajukuu kadhaa na anaendelea kuongoza Marekani katika muhula wake wa pili wa urais.

Safari yake kutoka katika familia tajiri ya wafanyabiashara, kupanua himaya ya majengo, kujijenga kupitia televisheni hadi kuingia katika siasa na kurejea Ikulu inaonesha namna alivyoweza kutumia umaarufu na uzoefu wake wa biashara kujenga nafasi katika siasa za Marekani.

Related articles

Recent articles