NYON, Uswis
ZIPO sababu kuu tatu zinazoweza kuisukuma FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa) kuipiga ‘stop’ timu ya taifa iliyo sehemu ya wanachama wake kushiriki fainali za Kombe la Dunia.
Moja ya hizo ni ubabe wa kivita dhidi ya wenzake. Pili, ni endapo taifa husika limewekewa vikwazo vya kimataifa. Tatu, ni Serikali kuingilia masuala ya soka.
Kwa sasa, Urusi ndiyo nchi pekee inayotumikia adhabu hiyo. Kwa msimu wa pili mfululizo (2022 na 2026), timu yake ya taifa haijagusa Kombe la Dunia.
Kilichoiponza Urusi ni uamuzi wa Serikali yake kuivamia kijeshi nchi jirani ya Ukraine. Vita vilianza mwaka 2022 na vimeendelea hadi leo hii.
Hivyo, Urusi inaungana na mataifa mengine 12 yaliyowahi kuzuiwa kwa nyakati kushiriki michuano iliyoasisiwa mwaka 1930.
Ujerumani na Japan zilizuiwa kushiriki fainali za mwaka 1950 baada ya kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia mwaka 1945.
Afrika Kusini nayo iliwekewa katazo la kucheza Kombe la Dunia kuanzia mwaka 1970 hadi 1990, sababu ikiwa ni ubaguzi wa rangi uliokuwa umetamalaki nchini humo chini ya Serikali ya kikoloni.
Pia, Mexico ilizuiwa kutia mguu katika michuano ya mwaka 1930 kutokana na skendo ya wachezaji wake kudanganya umri.
Haijasahaulika pia, kwamba Yugoslavia iliondoshwa kushiriki fainali za mwaka 1994, sababu ikiwa ni vikwazo ilivyokuwa imewekewa na Umoja wa Mataifa (UN).
Ni mwaka ambao Libya nayo ilizuiwa, sababu ikiwa ni hiyo hiyo, vikwazo kutoka UN.
Ni fainali ambazo Chile nayo ilipigwa pini kucheza baada ya kipa wao kumdanganya mwamuzi kuwa ameumia wakati wa mechi za kufuzu.
Kama itakumbukwa, Myanmar nayo ilizuiwa kuwa sehemu ya fainali za mwaka 2006 baada ya kugomea kucheza mechi ya kufuzu.
Timu ya Taifa ya Brunei iliwekewa katazo kucheza Kombe la Dunia 2014 kwa kosa la Serikali kuingilia masuala ya chama chake cha soka.
Vilevile, Zimbabwe iliondoshwa katika mechi za kufuzu fainali za mwaka 2018 baada ya kushindwa kulipa deni la mmoja ya makocha wao wa zamani.
Wakati huo huo, Indonesia na Kuwait zilizuiwa kwenye michuano hiyo iliyofanyika Urusi kwa kosa la serikali kuingilia masuala ya soka.


