LONDON, Uingereza
SIKU chache zilizopita, ulimwengu wa soka ulimpoteza binadamu aitwaye Ken Bates, ambaye alifariki akiwa na umri wa miaka 94.
Bates aliwahi kuimiliki Chelsea kwa miaka zaidi ya 20, akiinunua kwa Pauni milioni moja tu mwaka 1982, kabla ya kuvuna Pauni milioni 140 alipomuuzia tajiri wa Urusi, Roman Abramovich, mwaka 2003.
Hata hivyo, safari yake haikuanzia Chelsea. Aliwahi kuwa Mwenyekiti wa klabu ya soka ya Oldham Athletic katika miaka ya 1960.
Kabla ya kuinunua Chelsea, Bates alikuwa mmiliki wa Wigan Athletic katika miaka ya 1980.
Baada ya kuiacha Blues mikononi mwa Abramovich, Bates alikuwa mmoja ya wamiliki wa Leeds United kuanzia mwaka 2005 hadi alipoondoka klabuni hapo mwaka 2013.
ALIVYOIOKOA CHELSEA
Alipoinunua Chelsea, Bates aliikuta klabu hiyo ikiwa hoi kiuchumi. Kwa ufupi, aliikuta ikiwa na deni la Pauni milioni 1.5.
Aliweza kulipa na kuifanya kuwa moja ya klabu kubwa, akiiwezesha kutwaa ubingwa wa FA (mara mbili), Kombe la Ligi, Kombe la Washindi barani Ulaya (Ligi ya Mabingwa), na UEFA Super Cup.
Chini yake, alisajili wachezaji waliokuja kuwika Ligi Kuu ya England, wakiwamo Gianfranco Zola, Ruud Gullit, Marcel Desailly, Gianluca Vialli, Pat Nevin, Kerry Dixon na David Speedie.
Nje ya hapo, Bates anabaki kwenye vitabu vya historia ya Chelsea kama mmiliki aliyejenga Uwanja wa Stamford Bridge.
MATUKIO YAKE YA UTATA
Mwaka 1985, Bates aliweka uzio wa umeme wenye urefu wa futi 12 katika Uwanja wa Stamford Bridge, lengo likiwa ni kuwadhibiti mashabiki wakorofi.
Hata hivyo, akiwa ameshakamilisha ujenzi, mamlaka za Jiji la London zilimzuia kutumia uzio huo kwa sababu za kiusalama.
Mwaka 1995, alikorofishana na aliyekuwa Mkurugenzi, Matthew Harding, ambapo alimpiga marufuku kukanyaga klabuni hapo.
Harding alikuwa shabiki wa kutupwa wa Chelsea, ikifikia hatua ya kutoa pesa zake mfukoni kusaidia maboresho ya Uwanja wa Stamford Bridge na kusajili wachezaji.
Mwaka 1998, msimu mmoja baada ya ubingwa wa FA, Bates alimfuta kazi kocha Gullit. Alifukuzwa kwa meseji tu.
Vialli alichukua nafasi yake na kuipa Chelsea mataji mawili, lakini naye alifukuzwa msimu uliofuata na kusababisha Bates akosolewe vikali.
Kocha wa mwisho kuajiriwa na Bates kabla ya Abramovich kuinunua Chelsea alikuwa ni Claudio Ranieri.


