TORONTO, Canada
WAKATI huu fainali za Kombe la Dunia zikiendelea Marekani, Mexico na Canada, jina la kinda Nestory Irankunda limeandika historia mpya katika michuano hiyo.
Ni baada ya mshambuliaji huyo wa Watford mwenye umri wa miaka 20 kuwa mchezaji mdogo zaidi kufunga bao katika mechi ya Kombe la Dunia.
Aliweka rekodi hiyo alipoifungia Australia bao la kwanza katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Uturuki katika mchezo uliochezwa mjini Vancouver.
Irankunda alizaliwa mwaka 2006 katika kambi ya wakimbizi nchini Tanzania baada ya wazazi wake kukimbia machafuko vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Burundi.
Akiwa mdogo, alihamia Australia na wazazi wake na huko ndiko alikoanza safari yake ya soka kupitia ‘academy’ ya Adelaide United, kabla ya kupandishwa timu ya wakubwa ya Ligi Kuu (A-League).
Baada ya kiwango bora, akifunga mabao 16 na asisti nane, ndipo Bayern Munich ilipomsajili mwaka 2024, ingawa ilikuwa ngumu kwake kuingia kikosini cha kwanza.
Mwaka huo huo, aliitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha Australia, walipokutana na Bangladesh katika mchezo wa kufuzu fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia.
Katika mechi yake ya pili, Irankunda aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuifungia bao Australia. Alifanya hivyo dhidi ya Palestina.
Kutokana na kukosa nafasi ya kucheza Bayern, alijiunga na Grasshopper kwa mkopo msimu uliopita, kabla ya Watford kumsajili moja kwa moja.
Msimu uliomalizika, 2025-26, nyota huyo alicheza mechi 42 akiwa na timu hiyo ya Championship, akifunga mabao manne na kutoa asisti tano.


