26 C
New York

Kilimo cha bangi, uvutaji na madhara yake

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

KWA tafsiri ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya hapa nchini (DCEA), bangi ni aina ya dawa ya kulevya inayotokana na mmea unaoitwa ‘Cannabis sativa’, ambapo majani na maua yake hukaushwa na hutumiwa kama kilevi peke yake au kwa kuchanganywa na dawa zingine.

Mara nyingi bangi imekuwa ni kati ya dawa ya awali kutumiwa, ambapo watumiaji wengi huanza matumizi wakiwa na umri mdogo hivyo kuwa katika hatari zaidi kiafya, kijamii na kiuchumi.

Katika tovuti yake, DCEA inaeleza kuwa watumiaji wengi wa bangi huishia kutumia aina zingine za dawa za kulevya, zikiwamo ‘heroin’ na ‘cocaine’.

DCEA inatambua kuwa bangi imekuwa na majina kadhaa huko mitaani, ikiitwa pia ‘msuba’, ‘dope’, ‘nyasi’, ‘majani’, ‘mche’, ‘kitu’, ‘blanti’, ‘mboga’, ‘sigara kubwa’, ‘ndumu’, ‘msokoto’ na ‘ganja’.

KILIMO CHA BANGI

Mara nyingi hufanyika kwenye vyanzo vya maji, misituni na milimani ambapo miti hukatwa au kuchomwa moto na kusababisha kutoweka kwa baadhi ya viumbe hai na uoto wa asili, kukauka kwa vyanzo vya maji, mmomonyoko wa udongo na hatimaye ukame. Uharibifu huu umejidhihirisha katika safu za milima ya Uluguru, Usambara, Udzungwa na maeneo ya Arumeru.

Kushamiri kwa kilimo haramu cha bangi, kunaweza kusababisha uhaba wa mazao ya chakula na hivyo kupelekea kupanda bei ya vyakula na hata janga la njaa.

Kutokana na athari za matumizi na kilimo haramu cha bangi, Taifa linaingia gharama kubwa katika kukabiliana na tatizo hili, ikiwemo utoaji wa elimu mashuleni na katika jamii, matibabu ya maradhi mbalimbali, uteketezaji mashamba na udhibiti wa biashara haramu ya bangi.

Bangi huchangia kuongezeka kwa umasikini kwa mtumiaji, jamii na taifa kwa ujumla na kupelekea kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.

MADHARA YA BANGI

DCEA inaeleza kuwa bangi huamsha magonjwa ya akili, hususani msongo wa mawazo, achilia mbali moshi wake kuzalisha lami na kemikali mbalimbali zinazosababisha saratani ya mapafu.

Vilevile, bangi huathiri mifumo ya fahamu na kumfanya mtumiaji awe kwenye hali ya njozi ambapo ataona na kusikia vitu tofauti na uhalisia.

Hali hii inachangia kupunguza stamina ya mtumiaji na kusababisha ajali, uharibifu wa mali pamoja na kushusha ufanisi wa kazi.

Baadhi ya watumiaji hupata wasiwasi mkubwa mara wavutapo na kuwahisi vibaya watu wanaowazunguka kuwa wanataka kuwadhuru au kuhisi wanajua kuwa wamevuta bangi.

Matumizi ya bangi pia husababisha mapigo ya moyo kuongezeka na mishipa ya damu kupanuka na hata kusababisha kiharusi.

Kama hiyo haitoshi, uvutaji wa bangi huweza kusababisha kikohozi sugu, kukosa pumzi, vidonda vya koo, pumu, vitendo vya uhalifu ikiwemo wizi, utapeli na ukatili wa kijinsia katika jamii.

SHERIA ZINASEMAJE?

DCEA inafafanua kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, sura ya 95, kilimo na biashara ya bangi katika Taifa letu ni kosa la jinai.

Hivyo basi, kujihusisha kwa namna yoyote na bangi (kulima, kuuza, kuhifadhi, kutumia, kuichakata, n.k.) ni kosa la jinai na adhabu yake inafikia hadi kifungo cha maisha jela.

Related articles

Recent articles