28.1 C
New York

James Milner: Miaka 24 ya mataji, rekodi za aina yake EPL

Published:

LONDON, Uingereza

HATIMAYE kiungo mkongwe Ligi Kuu ya England (EPL), James Milner, alitangaza kustaafu soka hivi karibuni. Ni baada ya miaka 24 ya kucheza kwa kiwango cha juu kwenye michuano hiyo.

Milner (40), ameweka wazi kuwa ataondoka Brighton na kutundika daluga atakapomaliza mkataba wake mwishoni mwa Juni, 2026.

“Baada ya misimu 24 ya kucheza Ligi Kuu ya England, nafikiri ni wakati sahihi sasa kwangu kufikia mwisho wa maisha yangu ya soka,” aliandika Milner katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram.

SAFARI YAKE YA SOKA

Milner alianza maisha yake ya soka akiwa na Leeds United (2002 – 2004), kabla ya baadaye kuzitumikia Newcastle United (2004 – 2008), Aston Villa (2005-06, 2008-10), Manchester City (2010 – 2015), na Liverpool (2015 – 2023) kisha Brighton (2023 – 2026).

“Kila klabu niliyopitia imekuwa na mchango mkubwa katika maisha yangu ya soka, hivyo niwashukuru wote; kuanzia wamiliki, wafanyakazi, makocha, wachezaji wenzangu na mashabiki walionipokea na kunisaidia kufika hapa,” amesema.

Kwa ngazi ya timu ya taifa, alianza kuitumikia England ‘Three Lions’ mwaka 2009 hadi mwaka 2016, akicheza jumla ya mechi 61 akiwa na kikosi hicho.

Akiwa na England, Milner alishiriki mara mbili fainali za Mataifa ya Ulaya (EURO), kama ilivyokuwa kwa Kombe la Dunia.

Kwa EURO, alicheza jumla ya mechi tano (2012 na 2016), na upande wa Kombe la Dunia ni mechi nne (2010 na 2014).

MATAJI, REKODI ZA KUTOSHA

Milner amestaafu akiwa na mataji 13, yakiwamo matatu ya Ligi Kuu ya England; mawili akicheza Manchester City na moja alipohamia Liverpool.

Kama hiyo haitoshi, ni mshindi wa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya alilobeba akiwa na kikosi cha Liverpool mwaka 2019.

Mataji mengine ni FA (2), EFL (2), Ngao ya Jamii (2), UEFA Super Cup, UEFA Intertoto Cup, na Kombe la Dunia kwa ngazi ya Klabu.

Februari, 2026, nyota huyo aliweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi (658) za Ligi Kuu hiyo ya England.

Kwa upande mwingine, anaendelea kuwa mmoja ya wachezaji 10 (Top 10) wanaoongoza kwa pasi za mabao ‘asisti’ katika historia ya Ligi hiyo. Ana asisti 90.

Hata hivyo, ndiye mchezaji aliyetoa asisti kwa wachezaji wengi tofauti. Jumla ya wachezaji 47 walifunga mabao kwa asisti zake.

Wakati huo huo, Milner atakumbukwa kwa rekodi yake ya kuwa mchezaji wa kwanza mwenye umri mdogo zaidi (miaka 16) kufunga bao katika mechi ya Ligi Kuu ya England.

Pia, ni miongoni mwa wachezaji wawili pekee wenye umri mkubwa kufunga bao EPL. Alifanya hivyo akiwa na miaka 39 na siku 239.

“Naachana na soka nikijivunia kumbukumbu nzuri zitakazobaki kwa kipindi chote cha maisha yangu. Soka limenipa mafanikio ambayo sikutarajia … Asante kwa kila aliyekuwa sehemu ya safari yangu,” amesema.

Related articles

Recent articles