28.1 C
New York

‘Fuso’ ana mlima mrefu kuinasua Prisons isipotee Ligi Kuu Bara

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

MOJA ya timu zinazopumulia mashine msimu huu wa Ligi Kuu Bara ni Tanzania Prison inayonolewa na beki wa kulia wa zamani wa timu hiyo, Yanga na Taifa Stars, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’.

Prison ambayo inashika nafasi ya 15 katika msimamo wa timu 16, imecheza mechi 25, ambapo imeshinda tano, sare tano na kufungwa mara 15.

Nsajigwa aliajiriwa na klabu yake hiyo ya zamani akitokea Transit Camp ya Ligi Daraja la Kwanza (Championship), ambayo alishaiongoza katika michezo 19.

Katika mechi hizo, Transit Camp ilishinda 11, sare nne na kupoteza nne, ikifunga mabao 26 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 17.

ALIRITHI MATATIZO

Februari 27, 2026, Nsajigwa alitambulishwa rasmi kuwa kocha mpya wa Prison akichukua nafasi ya Zeckediah Otieno raia wa Kenya.

Otieno alifungashiwa virago baada ya timu hiyo kutokuwa na mwenendo mzuri kwenye Ligi, ambapo katika mechi 14, ilishinda tatu, sare tatu na kufungwa nane.

Itakumbukwa kuwa kocha huyo aliondoka kwenye benchi la ufundi wakati timu hiyo ikiwa nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi baada ya kukusanya pointi 12 tu kati ya 42 ilizopaswa kuwa nazo.

Kwa maana hiyo, Nsajigwa aliikuta Prison tayari ikiwa na changamoto, hivyo alianza kazi kwenye presha kubwa, labda tofauti na ambavyo angeanza nayo msimu.

TAKWIMU ZAKE KWENYE BENCHI

Licha ya Nsajigwa kuajiriwa Februari, mechi yake ya kwanza ya Ligi akiwa kocha mkuu wa Prison ilichezwa Machi 5, 2026, akianza na suluhu (0-0) dhidi ya matajiri wa Chamazi, Azam.

Tangu hapo, ameiongoza timu hiyo katika mechi zingine 10 za Ligi lakini ameshinda mbili pekee (1-0 dhidi ya Fountain Gate, 3-2 dhidi ya Pamba), sare moja (1-1 dhidi ya KMC) na kufungwa saba.

Kuziweka sawa takwimu, katika jumla ya mechi 11 alizokaa kwenye benchi, Prisons yake imefunga mabao saba na kuruhusu 19. Katika pointi 33 alizopaswa kuwa nazo katika mechi 11, Nsajigwa ameambulia nane pekee.

ATAINUSURU KUSHUKA DARAJA?

Timu nne ziko kwenye hatari ya kucheza ‘play-off’ au kushuka daraja moja kwa moja. Timu hizo ni Namungo inayoshika nafasi ya 13 kwa pointi 25, Mbeya City (nafasi ya 14, pointi 22), Prison (nafasi ya 15, pointi 20), na KMC (nafasi ya 16, pointi 9).

Kwa hesabu za kawaida, ukiacha KMC, ambayo kubaki kwake Ligi Kuu kutategemea uwezekano wa kupata play-off, timu zote tatu zilizobaki zina nafasi ya kuondoka katika mstari mwekundu endapo zitazitumia vizuri mechi tano zilizobaki.

Ikumbukwe, Mtibwa Sugar ambayo ndiyo iliyopo juu ya Namungo, Mbeya City na Prison ikiwa nafasi ya 12, ina pointi 27 tu, ambazo zinaweza kufikiwa na timu yoyote kati ya hizo tatu.

Kwa Nsajigwa, michezo iliyobaki kujinusuru na play-off au kushuka daraja ni dhidi ya Dodoma Jiji (nyumbani, Juni 14, 2026), JKT (ugenini, Juni 18, 2026), Singida Black Stars (ugenini, Juni 24, 2026), Mtibwa Sugar (nyumbani, Juni 27, 2026), na Mashujaa (Juni 30, 2026).

Related articles

Recent articles