19.8 C
New York

Depu na kivuli cha Dube: Yanga inahitaji straika mpya?

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

MJADALA wa kiwango cha mashambuliaji wa kimataifa wa Angola, Depu, tangu asajiliwe na Yanga umeshika kasi mitandaoni na hata vijiweni, wengi wakijiuliza; ni usajili uliolipa au uliofeli?

Nyota huyo alijiunga na Yanga wakati wa dirisha dogo Januari, 2026, wakati huo ikionekana kwamba Prince Dube ameshindwa majukumu yake ya ushambuliaji. Hivyo, Depu alisajiliwa ili awe mbadala wake.

Kinyume chake, Depu ameishia kuwa mchezaji wa akiba na wakati mwingine kukosekana kabisa kwenye benchi, huku Dube akionekana kupewa nafasi kubwa zaidi ya kucheza.

TAKWIMU BADO ZINAMBEBA

Kama ni takwimu za Ligi Kuu Bara, basi Depu bado ni mchezaji wa kiwango kizuri Yanga. Ana miezi takribani mitano tu kikosini, amecheza mechi 12 na kufunga mabao sita na kutoa ‘asisti’ mbili.

Kwa namba hizo, huwezi kusema Depu ni mshambuliaji asiye na kiwango cha kucheza Yanga au klabu yoyote ya Ligi Kuu Bara. Takwimu zinamlinda.

Wakati huo huo, katika miezi mitano hiyo, ametumia muda mwingi kuuguza majeraha. Ni wachezaji wachache wanaoweza kurudi na moto ule ule baada ya kupona majeraha. Apewe muda.

Ukimlinganisha na Dube, mwenzake huyo alianza msimu huu akiwa na Yanga, hivyo amecheza mechi 19 za Ligi Kuu Bara. Akikosa zingine kutokana na majeraha. Katika michezo hiyo, amefunga mabao tisa na kutoa asisti nne.

Kwa hesabu za kawaida, licha ya kuzidiwa mechi saba na Dube, Depu amebakiza mabao matatu tu na asisti mbili kumfikia straika huyo wa kimataifa wa Zimbabwe.

Vipi endapo Depu angekuwa anapata muda wa kucheza kama ilivyo kwa Dube? Vipi wote wangeanza pamoja msimu huu wa Ligi Kuu Bara? Ni wazi namba za mabao na asisti zingekuwa tofauti.

TATIZO LIKO HAPA

Aina ya uchezaji ndiyo inayomfanya Depu asiwe kipaumbele kwa benchi la ufundi la Yanga. Licha ya uzuri wake, kama takwimu zinavyoeleza, amekuwa akisubiri huduma zimfuate kwenye boksi ili afunge.

Ni tofauti na Dube, ambaye uwezo wake wa kuzunguka katika eneo la mwisho umekuwa ukiivuruga ‘shepu’ ya safu ya ulinzi ya wapinzani na kuilazimisha ifanye makosa.

Pia, tofauti na Depu, Dube ni mzuri katika ‘pressing’, yaani kufuatilia mipira inayochezwa kati ya kipa na mabeki wa timu pinzani. Dube anapokuwa uwanjani, huzifanya timu nyingi kushindwa kupanga mashambulizi yanayoanzia kwa kipa.

Ni kwa maana hiyo, kati ya washambuliaji hao, Dube amekuwa akipewa nafasi kubwa na benchi la ufundi la Yanga kutokana na mchango wake wa kucheza hata pale timu inapokuwa haina mpira. Atakaba kuanzia kwenye boksi na kutengeneza nafasi au kufunga.

YANGA INAHITAJI STRAIKA MPYA?

Kwa takwimu, bado haziridhishi kusema Dube ana utofauti mkubwa na Depu. Tofauti ya mabao matatu na asisti mbili akiwa amecheza mechi saba zaidi (za Ligi), bado inapaswa kumfikirisha Dube katika majukumu yake ndani ya uwanja.

Licha ya sifa tajwa hapo juu, Dube amekuwa akipoteza nafasi nyingi za kufunga, ambazo mshambuliaji wa daraja lake na matarajio ya Yanga, alipaswa kuzitumia kufunga mabao.

Iko wazi, kwamba kwa namna Yanga inavyotengeza nafasi nyingi katika kila mchezo, huenda Dube angeshafikisha mabao zaidi ya 20 endapo angekuwa straika ‘katili’ katika kuzitumia.

Related articles

Recent articles