MERSEYSIDE, England
LIVERPOOL wametangaza kumfuata kazi kocha wao raia wa Uholanzi, Arne Slot. Ametimuliwa leo Mei 30, 2026, zikiwa ni siku 365 tangu alipoajiriwa.
“Klabu ya soka ya Liverpool inathibitisha kuachana na Arne Slot katika majukumu yake kama kocha mkuu na mchakato wa kupata mbadala wake unaendelea,” imeeleza taarifa ya Liverpool.
Wakati anaajiriwa miezi 12 iliyopita, matarajio ya Liverpool kwa kocha huyo yalikuwa makubwa, ikitokana na mafanikio aliyokuwa nayo akiwa kocha wa Feyenoord.
Katika msimu wake wa kwanza akirithi mikoba ya Jurgen Klopp, Slot aliiongoza Liverpool kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England (EPL) zikiwa zimebaki mechi nne.
Kuelekea msimu wake wa pili, Slot aliimarisha zaidi kikosi, akitumia Pauni milioni 446 zilizovunja rekodi ya matumizi ya sokoni katika historia ya soka la Uingereza.
Florian Wirtz alitua akitokea Bayer Leverkusen, kama ilivyokuwa kwa Alexander Isak, Hugo Ekitike, Hugo Ekitike, Jeremie Frimpong na Milos Kerkez.
Hata hivyo, licha ya usajili mzuri, wimbi la majeraha lilitibua kwa kiasi kikubwa mipango ya kocha huyo katika msimu wake wa pili Anfield.
Kwa nyakati tofauti, Slot aliwakosa nyota wake watatu tegemeo – kipa namba moja, Alisson Becker, straika Isak na winga Wirtz – kutokana na majeraha.
Katika mazingira yaliyoonesha ubovu wa Liverpool ya Slot kwa msimu wa 2025-26, timu hiyo haikuifunga timu yoyote iliyopanda daraja pale Anfield.
Hatimaye, ilimaliza Ligi ikiwa nafasi ya tano kwenye msimamo baada ya kushinda mechi 17, sare tisa, kufungwa 12 na kukusanya pointi 60 pekee, ikizidiwa 25 na mabingwa Arsenal.
Baada ya kufukuzwa, kocha anayepewa nafasi kubwa ya kuvaa viatu vyake ni Andoni Iraola wa Bournemouth, kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa Italia anayeaminika kwa taarifa sahihi za usajili, Fabrizio Romano.


