LONDON, Uingereza
MSIMU wa 2025-26 haukuwa mzuri tu kwa Arsenal, bali pia umeacha alama kubwa katika safari ya soka la kulipwa ya kinda wao raia wa England, Max Dowman.
Kutokana na kiwango chake msimu huu, Dowman mwenye umri wa miaka 16 ndiye aliyetwaa tuzo ya Kinda Bora wa Mwaka wa Ligi Kuu ya England (EPL).
Katika mechi yao ya mwisho dhidi ya Crystal Palace, Dowman aliandika historia ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kuingia ‘first eleven’ ya mechi za Ligi Kuu ya England (EPL).
Akiwa na miaka 16 na siku 144, ‘dogo’ huyo alivunja rekodi iliyodumu EPL kwa miaka 18, tangu Jose Baxter alipoweka akiwa na Everton mwaka 2008, ambapo aliingia kikosi cha kwanza katika mchezo dhidi ya Blackburn Rovers.
Itakumbukwa, rekodi hiyo iliwahi kuwekwa na Wayne Rooney aiwa na Everton mwaka 2002, ambapo alianza katika mchezo dhidi ya Tottenham akiwa na umri wa miaka 16 na siku 297.
Novemba, 2025, aliandika historia ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya. Miaka 15 na siku 308, akitokea benchi katika mchezo dhidi ya Slavia Prague.
Machi, 2026, Dowman aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kucheza na kufunga bao katika historia ya EPL.
Alifanya hivyo akitokea benchi katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Everton, ambapo aliingia uwanjani katika dakika ya 75.
Kwa upande mwingine, Dowman anakuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kutwaa taji la EPL, akiivunja rekodi ya Phil Foden.
Kabla ya Dowman, Foden aliandika historia hiyo Manchester City ilipochukua ubingwa msimu wa 2017-18, wakati huo akiwa na miaka 17 na siku 350.
Kwa Arsenal, mchezaji wa mwisho kutwaa ubingwa wa EPL akiwa ‘bwana mdogo’ ni Gael Clichy – miaka 18 na siku 294, msimu wa 2003-04.
Dowman alizaliwa Desemba 31, 2009, mjini Chelmsford, Essex. Anatokea familia yenye mashabiki wengi wa Arsenal. Babu yake, George Male, aliwahi kuitumikia klabu hiyo miaka mingi iliyopita.
Alianza maisha yake ya soka akiwa na timu ya mtaani, Billericay Town, kabla ya kujiunga na ‘academy’ ya Arsenal alipokuwa na umri wa miaka nane mwaka 2015.
Ameshafunga bao moja katika mechi sita alizocheza tangu kocha Mikel Arteta alipompandisha timu ya wakubwa mwaka 2025.
Kwa ngazi ya timu ya Taifa ya England, Dowman ameshatumikia U-16, U-17 na U-19, akifunga jumla ya mabao saba katika mechi 31.
Novemba, 2025, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuifungia bao timu ya U-19 ya England.
Dowman bado ni mwanafunzi na kwa mujibu wa kanuni za EPL, amekuwa akitumia chumba tofauti cha kubadilisha nguo (iwe mazoezini au kwenye mechi) kutokana na umri wake.


