Na mwandishi wetu, Gazetini
WATOTO wa mjini wakikwambia ‘utaacha ndala’, huwa wanamaanisha utakutana na kitu kizito. Je, ni mashabiki wa Yanga au Simba watakaokutwa na kitu kizito?
Baada ya kuifunga Mwembe Makumbi mabao 4-0, Yanga iliifunga Azam mabao 2-1 katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex.
Kwa upande wao, Simba ‘Wekundu wa Msimbazi’ waliifunga Mafunzo bao 1-0, kabla ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mlandege FC katika mechi ya nusu fainali.
Hivyo, vigogo wa soka la Tanzania, Yanga na Simba, wataitikisa Zanzibar katika mchezo wa fainali utakaochezwa Aprili 29, 2026 katika Uwanja huo.
Kwamba taji la msimu huu wa Kombe la Muungano litaangukia Tanzania Bara baada Mlandege kulibakiza Visiwani Zanzibar msimu uliopita.
Si Simba, wala Yanga, kila timu imeonesha uwezo mkubwa wa kufifumania nyavu katika mechi mbili zilizopita.
Yanga wana mabao sita ya kufunga, wastani wa mabao matatu kwa kila dakika 90, wakati Simba wao wana manne, sawa na mawili katika kila dakika 90.
Pia, timu zote zimeonekana kuwa na ubora mkubwa katika eneo la ulinzi. Yanga imeingia fainali ikiwa imefungwa bao moja pekee, huku Simba ikiwa haijaruhusu nyavu zake kutikiswa.
Je, rekodi nazo zinasemaje? Katika ‘Kariakoo derby’ tano zilizopita, Simba haijaweza kuchomoza na ushindi, na badala yake Yanga imeshinda mara nne na kutoa sare moja.
Sare hiyo ya kutokufungana ilipatikana katika mechi ya mzunguko wa kwanza msimu huu wa Ligi Kuu Bara iliyochezwa Machi Mosi, 2026.


