RIYADH, Saudi Arabia
LICHA ya mkataba wake kumalizika mwaka 2027, huenda Cristiano Ronaldo akaondoka Al-Nassr mwishoni mwa msimu huu wa 2025-26.
Taarifa zilizopo zinadai kuwa nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ureno ametibuana na mabosi wa Al-Nassr na ndiyo maana aligoma kucheza mechi iliyopita dhidi ya Al-Riyadh.
Je, ni wapi ataelekea ‘CR7’ endapo itatokea akaondoka Ligi Kuu ya Saudi Arabia mwishoni mwa msimu huu?
Marekani
Mwaka 2023, mshambuliaji huyo wa zamani wa Manchester United, Real Madrid na PSG alisema Ligi Kuu ya Marekani (MLS) ni bora kuliko ile ya Saudi Arabia.
Kwa mashabiki wa soka, wanasubiri kuona kama Ronaldo atamfuata mpinzani wake mkubwa, Lionel Messi, ambaye yuko MLS akiitumikia Inter Miami.
Sporting Lisbon
Huenda Ronaldo akaona huu ni wakati sahihi kwake kwenda kumalizia soka lake katika klabu hiyo iliyoibua kipaji chake.
Hata hivyo, mwaka 2025 alisema hafikirii kurudi Ulaya hivi karibuni. Je, atabadili mawazo na kurejea nyumbani?
Saudi Arabia
Inawezekana pia kwa Ronaldo kujiunga na klabu nyingine ya Saudia. Kama ataondoka Al-Nassr, basi atajiunga na klabu nyingine inayomilikiwa na Mfuko wa Uwekezaji wa Saudi Arabia.
Je, ni ipi kati ya Al-Hilal na Al-Ahli na Al-Ittihad? Mfuko huo (PIF) unamiliki asilimia 75 ya hisa katika klabu hizo. Karim Benzema aliondoka Al-Ittihad na kutua Al-Hilal.
Real Madrid
Ronaldo ni lejendari wa Madrid kwa mafanikio makubwa aliyowapa kabla ya kuondoka mwaka 2018 na kutua Juventus.
Huenda ikawa ngumu lakini mashabiki wa Madrid wangependa kuona Ronaldo akicheza ‘pacha’ na Kylian Mbappe katika eneo la ushambuliaji.
Chelsea
Kabla ya kutimkia Al-Nassr akitokea Manchester United, Chelsea walijaribu kuinasa saini ya mshambuliaji huyo.
Safari hii, licha ya Chelsea kuendelea wachezaji wenye umri kati ya miaka 16 na 25, huenda wanavutiwa na uzoefu mkubwa alionao CR7.
Newcastle
Kutokana na ukaribu na uhusiano mzuri uliopo kati ya Newcastle United na Saudi Arabia, lolote linaweza kutoka. Ronaldo kutua na St. James Park.
Kama haijasahaulika, mabosi wa Newcastle United nao waliingia vitani kujaribu kumsajili mchezaji huyo wakati alipoondoka Old Trafford.


