Na mwandishi wetu, Gazetini
KLABU ya Yanga leo Alhamisi Januari 15, 2026, imemtambulisha straika wa kimataifa wa Angola, Laurindo Dilson Maria Aurelio ‘Depu’, kupitia kurasa zake za mitandaoni ya kijamii.
Nyota huyo aliyezaliwa mwaka 2000, amenaswa na vigogo hao wa Ligi Kuu Bara akitokea Radomiak Radom ya Poland. Wafuatiliaji wa michuano ya COSAFA watakumbuka kuwa Depu alikuwa mfungaji bora wa michuano hiyo mara mbili mfululizo (2024 na 2025).
Safari yake Ulaya
Historia yake ya kucheza soka barani Ulaya inaanzia mwaka 2023, ambapo alisajiliwa na klabu ya Gil Vicente ya Ureno kwa mkataba wa miaka mitatu na nusu.
Mwaka 2024, baada ya kuonesha kiwango kizuri akiwa na timu ya taifa ya Angola kwenye michuano ya COSAFA, Depu alisajiliwa na Vojvodina ya Serbia.
Akiwa kwa mkopo wa mwaka mmoja, nyota huyo alikuwa sehemu ya kikosi kilichofika fainali ya Kombe la Ligi msimu wa 2024-25, ingawa walifungwa na vigogo Red Star Belgrade.
Hata hivyo, takwimu binafsi hazikuwa nzuri kwake kwani alitoa ‘asisti’ moja pekee katika mechi 17 alizoshuka dimbani. Juni 30, 2025, Depu aliondoka klabuni hapo na kujiunga na Radomiak Radom ya Poland kwa mkataba wa miaka mitatu.
Wakati huo, akitoka kuwa mfungaji bora wa COSAFA kwa mabao nane katika mechi tano, saini yake ilikuwa ikiwaniwa na vigogo kadhaa wa soka la Afrika, zikiwamo Orlando Pirates na Kaizer Chiefs.
Anaipambania familia yake
Katika kila mafanikio, basi nyuma yake kuna historia ya jasho na damu. Katika moja ya mahojiano yake, Depu aliwahi kusimulia ilivyokuwa ngumu kwake kufikia mafanikio aliyonayo.
“Baba alikimbia na kutuacha nikiwa na umri wa miaka 14 tu. Kwa hiyo, mama alibeba jukumu la kutulea mimi, kaka zangu wawili, dada na binamu yangu.
“Najitoa kwa ajili yake. Nacheza soka kwa ajili ya kuisaidia familia yangu. Ipo siku nitamtafuta baba yangu lakini najua ananisoma kupitia magazeti na ameniona kupitia televisheni,” alisema Depu.
Apewa viatu vya Boyeli
Usajili wake, ambao vyanzo kadhaa vya habari vinaeleza kuwa umeigharimu Yanga kitita cha Sh milioni 619, umelenga kuziba pengo la mshambuliaji Andy Boyeli aliyerejea Shekhukhune ya Afrika Kusini.
Boyeli aliyekuwa Yanga kwa mkopo, alishindwa kulishawishi benchi la ufundi la Wanajangwani hao kutokana na kukosa mwendelezo wa makali ya kuzifumania nyavu.


