11.6 C
New York

Azam v Yanga; Ibenge dhidi ya ‘ukuta’ wa Goncalves

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

NI Yanga na Azam FC ndizo zitakazofunga pazia la msimu huu wa michuano ya Kombe la Mapinduzi huko Zanzibar. Timu hizo zitacheza fainali Jumanne ya Januari 13, 2026.

Mabingwa wa kihistoria Ligi Kuu Bara, Yanga, walijihakikishia nafasi ya kucheza fainali baada ya ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Singida Black Stars.

Bao pekee la mchezo huo wa nusu fainali uliochezwa katika Uwanja wa New Amaan Complex lilifungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa DRC, Maxi Nzengeli.

Kwa upande wao, matajiri wa Chamazi, Azam, wao walivuka hatua ya nusu fainali kwa ushindi kama huo (1-0) dhidi ya vigogo wenzao wa Ligi Kuu Bara, Simba.

Azam, ambao ni mabingwa mara tano wa Kombe la Mapinduzi, walipata bao pekee hilo kupitia kwa beki wake, Lameck Lawi, aliyecheka na nyavu za Simba katika dakika ya 73.

Yanga chini ya kocha raia wa Ureno, Pedro Goncalves, watashuka katika nyasi za Uwanja wa Gombani kuikabili Azam wakiwa na rekodi nzuri ya safu ya ulinzi msimu huu wa Kombe la Mapinduzi.

Takwimu zinaonesha kuwa Wanajangwani hao ndiyo timu pekee ambayo haijaruhusu nyavu zake kutikiswa baada ya kucheza mechi tatu.

Iko hivi; vijana hao wa Mitaa ya Jangwani na Twiga walifungua pazia kwa kuifunga KVZ mabao 3-0, kabla ya ushindi wa bao 1-0 katika mechi mbili zilizofuata (dhidi ya TRA na Singida Black Stars).

Je, Azam ya kocha mzoefu barani Afrika, Florent Ibenge, itakuwa timu ya kwanza kuzifumania nyavu za Yanga?

Aidha, Azam wamefika fainali wakiwa bao moja, licha ya kushinda mechi zote tatu dhidi ya Mlandege (2-0), URA (2-1) na Simba (1-0).

Katika mchezo huo wa fainali, Ibenge na vijana wake watakuwa wakisaka taji lao la sita katika historia ya mashindano hayo baada ya kuwa mabingwa mwaka 2012, 2013, 2017, 2018 na 2019.

Wakati huo huo, Yanga wanalifukuzia taji lao la tatu, ikikumbukwa kuwa vigogo hao ni mabingwa wa Kombe la Mapinduzi kwa mwaka 2007 na 2021.

Rekodi zao ziko hivi; katika mechi 23 walizokutana na Yanga, Azam imeweza kuchomoza na ushindi mara saba, ikifungwa 11 na kupata sare mara tano.

Mechi 23 hizo zimeshuhudia jumla ya mabao 53 yakifungwa, ambapo Yanga imepachika 27 na kuruhusu nyavu zake kuguswa mara 25.

Mara ya mwisho kwa vigogo hao kutoana jasho ilikuwa Aprili 10, 2025, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao dakika 90 zilimalizika kwa mwenyeji Azam kutandikwa mabao 2-1.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img