Na mwandishi wetu, Gazetini
RAIS Donald Trump ameweka wazi kuwa Marekani inakihitaji kwa namna yoyote ile kukiweka chini ya himaya yake Kisiwa cha Greenland.
Kauli hiyo ikamuibua Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, akimtaka Trump kuacha tamaa na vitisho.
Kwanini Denmark imeijibu Marekani? Kuna uhusiano gani kati ya Denmark na Greenland na kwanini Trump anakitaka Kisiwa hicho? Makala haya yanachambua zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari wikiendi iliyopita, Trump alisema Marekani inakihitaji Kisiwa cha Greenland kwa sababu za kiusalama.
Haikuwa mara ya kwanza kwa Trump kuonesha kuitaka Greenland. Mwaka 2019, alitangaza ofa ya kutaka kukinunua. Akaambiwa hakiuzwi.
Marekani ina kambi yake kubwa ya kijeshi katika Kisiwa hicho, hivyo kuacha kiwe karibu na mataifa mengine, hasa Urusi na China, kunahatarisha usalama wake.
Pia, kumiliki Greenland kutaifanya Marekani kuwa na uwanda mpana wa jeshi la majini, ilifahamika kuwa sehemu kubwa ya Kisiwa hicho inazi kutanisha bahari mbili kubwa za Atlantic na Arctic.
Wakati huo huo, Greenland ni Kisiwa tajiri kwa madini. Hapa yanazungumziwa madini adimu yanayotumika kutengeneza betri za simu, simu za kisasa, magari ya umeme na vifaa vingine vya kiteknolojia.
Ni madini ambayo China ndiyo mteja wake mkubwa, ikikumbukwa kuwa Taifa hilo la Asia lina ushindani mkubwa wa kiuchumi na Marekani.
Vilevile, baadhi ya wanasayansi wanadai kuwa Greenland ina utajiri wa rasilimali za mafuta na gesi, ambazo bado hazijaanza kutumika.
Je, kuna uhusiano gani kati ya Greenland na Denmark? Denmark imewahi kukitawala Kisiwa hicho kama koloni lake. Ni miaka zaidi ya 300 iliyopita.
Wakati wa Vita ya Pili ya Dunia, Ujerumani iliichukua Denmark na kuifanya koloni na ndipo Marekani ilipovamia Greenland na kuanzisha kambi ya jeshi na vituo vya redio.
Baada ya vita, vikosi vya Marekani vilibaki katika Kisiwa hicho. Mwaka 1951, Denmark iliipa Marekani jukumu la kusimamia ulinzi hapo Greenland.
Mwaka 1953, Greenland ikawa sehemu ya Denmark na raia wa Kisiwa hicho wakapewa urais wa nchi hiyo ya Ulaya.
Hata hivyo, Greenland ilijinasua kwenye minyororo ya ukoloni na kujitangazia uhuru wake mwaka 1979, ingawa bado Denmark imeendelea kuwa na mkono wake.
Denmark imekuwa ikimiliki sera za nje, ulinzi na usalama, huku pia uchumi wa Greenland ukiitegemea kwa kiasi kikubwa nchi hiyo ya barani Ulaya.
Hiyo ni pamoja na kupewa kiasi kikubwa cha fedha za msaada kila mwaka ili kugharamia huduma za kijamii, zikiwamo elimu na afya.
Je, Denmark ina uwezo wa kuzuia endapo Marekani itaamua kuivamia Greenland kama ilivyofanya kwa Venezuela siku chache zilizopita?
Ni wazi Denmark haina uwezo wa kijeshi kukabiliana na Marekani, ambayo inatajwa kuwa ndiyo nchi imara zaidi duniani katika eneo hilo.
Lakini je, wananchi wa Greenland wanasemaje? Wanavutiwa na upande upi? Kuwa sehemu ya Marekani, Denmark au kubaki wenyewe?
Baada ya Trump kusema Marekani inakitaka Kisiwa cha Greenland, Waziri Mkuu wa Kisiwa hicho, Nielsen, alijibu:
“Tuko tayari kwa mazungumzo, lakini yawe na misingi inayoheshimu sheria za kimataifa.”
Kwa upande mwingine, baadhi ya raia wamekasirishwa na kauli ya Trump wakisema wanataka kuiona nchi yao ikijitawala bila shinikizo.
Hata hivyo, wapo wanaoamini kuwa nchi yao itakuwa salama chini ya Denmark, ingawa pia wengine wanasema Marekani ni upande sahihi zaidi.


