Na mwandishi wetu, Gazetini
USHINDWE wewe tu! Sasa mashabiki na wanachama wa Simba wanaweza kupata jezi zao kidigitali, hata kupitia simu zao za mkononi.
Wakati huo huo, hatua hiyo inaambatana na punguzo kubwa la bei ya jezi za msimu huu, kutoka Shilingi 45,000 hadi Shilingi 12,000.
Ofa hiyo ya siku 45 imeanza leo Desemba 16, 2025, na ni kwa jezi zote, kwa maana ya zile za Ligi Kuu, michuano ya kimataifa, pamoja na za watoto.
Akizungumza katika Mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally, amesema:”Kupitia mitandao ya simu, unaweza kununua (jezi) ukitumia mtandao wowote ukilipa kwa namba ya 61223807 na baada ya hapo utakwenda kwenye ofisi ya Shirika la Posta au ofisi za JayRutty kuichukua.”
Juu ya punguzo la bei, Ally amesema ofa hiyo ni katika kuwapatia mashabiki, wanachama na wapenzi wa Simba zawadi ya Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
“Katika kipindi kama hiki, wafanyabiashara wengi wanatoa ofa kwa wateja wao kwa sababu mahitaji yanakuwa mengi. Kwa sababu hiyo, sisi kama Simba kwa kushirikiana na JayRutty tunaona twende sawa na dunia inavyokwenda,” amesisitiza.
Kwa upande mwingine, Ofisa Habari huyo ameongeza kuwa ofa hiyo ni sehemu ya kampeni ya klabu yao kupambana na biashara ya mauzo ya jezi feki.
“Kama Mwanasimba alikuwa ananunua jezi feki kwa Shilingi 15,000, sasa ‘original’ ataipata kwa Shilingi 12,000. Uamuzi ni wako Mwanasimba,” amesema.


