CAIRO, Misri
FAINALI za mwaka huu za Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) zinatarajiwa kuanza kutimua vumbi lake Desemba 21, mwaka huu, na zitafikia ukomo Januari 18, mwakani.
Uchambuzi unaliangazia Kundi C, ambalo linazikutanisha Nigeria, Tanzania, Tunisia na Uganda.
Nigeria ‘Super Eagles’ watashiriki kwa mara ya 21 fainali hizo. Ikumbukwe, hao ni mabingwa mara tatu, wakifanya hivyo katika miaka ya 1980, 1994 na 2013.
Msimu uliopita, 2023, vigogo hao wa soka la Afrika walikaribia kabisa kubeba tena taji hilo lakini walipoteza mchezo wa fainali.
Kwa upande wa Tanzania ‘Taifa Stars’, hii ni mara yao ya nne kushiriki AFCON. Ni baada ya kufanya hivyo katika miaka ya 1980, 2019 na 2023.
Safari hii, Taifa Stars itakwenda Morocco ikisaka rekodi kubwa mbili. Mosi, ni kushinda mechi ya kwanza katika michuano hiyo. Pia, ni kuvuka hatua ya makundi.
Tunisia ‘Eagles of Carthage’ watashiriki AFCON kwa mara ya 22. Kama itakumbukwa, hao ni mabingwa mara moja (2004).
Msimu uliopita, 2023, Tunisia iliishia hatua ya makundi baada ya kufika robo fainali katika michuano ya mwaka 2021.
Wakati huo huo, Uganda ‘The Cranes’ watakumbuka kuwa mafanikio yao makubwa zaidi katika mashindano hayo ni kufika fainali mwaka 1978.
Hii ni mara yao ya tisa kushiriki fainali za AFCON lakini ni ya tatu tu tangu walipofika fainali na kufungwa mabao 2-1 na Ghana.
Msimu uliopita, 2023, Uganda waliishia hatua ya 16 Bora. Kabla ya hapo, kwa maana ya fainali za mwaka 2017, safari yao ilikwamia hatua ya makundi.
Published:


