LONDON, Uingereza
CHELSEA watakuwa nyumbani Stamford Bridge kesho kuwaalika Arsenal katika mchezo wa Ligi Kuu, ambao ni ‘derby’ Jiji la London.
Arsenal wanaongoza Ligi wakiwa na pointi 29, wakati Blues wako nafasi ya pili wakiwa wameachwa pointi 23, huku kila timu ikiwa imeshacheza mechi 12.
Timu hizo zinakutana zikiwa kwenye viwango bora, ambapo Chelsea iliifunga Barcelona mabao 3-0, wakati Arsenal waliitandika Bayern mabao 3-1.
Kwa upande mwingine, Anthony Taylor ndiye mwamuzi wa kati aliyeteuliwa kuchezesha dakika 90 hizo.
Kwa kocha huyo mwenye umri wa miaka 47, hiyo itakuwa mechi yake ya 413 ya Ligi Kuu.
Katika mechi hizo, mzaliwa huyo huyo wa jijini Manchester ametembeza kadi za njano 1,446 na zile nyekundu za moja kwa moja ni 36, achilia mbali 22 zilizotokana na njano mbili.
Taylor amechezesha mechi 10 za Ligi Kuu msimu huu na amegawa kadi za njano 31, ingawa bado hajatoa nyekundu.
Lakini, kwa msimu huu, mwamuzi huyo amegawa penalti mbili pekee na zote ni katika mechi ambayo Sunderland iliifunga Brentford mabao 2-1.
Tangu msimu huu uanze, Taylor amechezesha mechi moja ya Chelsea. Blues waliifunga Liverpool mabao 2-1.
Pia, amechezesha moja ya Arsenal, ambapo Washika Bunduki waliifunga Fulham bao 1-0.
Takwimu za jumla zinaonesha kuwa Taylor amechezesha jumla ya mechi 56 za Chelsea. Blues imeshinda 29, imefungwa 13 na sare 14.
Wakati huo huo, Arsenal imeshinda 32 na kupoteza nane tu kati ya 56 ilizowahi kuchezeshwa na mwamuzi huyo.
Published:


