8.4 C
New York

Arsenal ya Arteta na takwimu za kibabe

Published:

LONDON, Uingereza
USHINDI wa mabao 3-1 dhidi ya Bayern Munich ni ujumbe mzito wa Arsenal kwa wapinzani wao msimu huu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na hata Ligi Kuu ya England (EPL).
“Kwanza, napaswa kuwapongeza wachezaji wetu kwa sababu walicheza vizuri, tena dhidi ya timu bora zaidi kwa sasa barani Ulaya,” alisema kocha wa Arsenal, Mikel Arteta.
Takwimu zinaongea
Takwimu ziko wazi, kwamba Arsenal ya Mhispania huyo imekuwa moto wa kuotea mbali msimu huu, ambapo kati ya mechi 19 zilizopita, imeshinda 16, sare mbili na kufungwa moja.
Kwa upande wa Ligi ya Mabingwa, Washika Bunduki hao wa London wameshinda mechi zote tano, ikiwa ni mara ya kwanza kwao kuwa na kasi hiyo tangu walipofika fainali msimu wa 2005-06.
Wamaliza unyonge kwa Bayern
Dhidi ya Bayern, vijana hao wa Mikel Arteta wamemaliza ‘uteja’ wao wa muda mrefu mbele ya vigogo hao wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).
Kabla ya mechi hiyo iliyochezwa Emirates, Arsenal ya Kaskazini mwa Jiji la London haikuwa imepata ushindi mbele ya Wajerumani hao tangu mwaka 2015.
Kama hiyo haitoshi, kabla ya mechi hiyo, Bayern haikuwa imepoteza mechi msimu huu wa Bundesliga na michuano yote wanayoshiriki.
Kiungo wa Arsenal, Declan Rice, ndiye aliyeibuka nyota wa mchezo huo. “Ukiitazama Bayern Munich msimu huu, wana timu Bora sana msimu huu. Ilikuwa mechi ngumu zaidi kucheza msimu huu,” alisema.
Kikosi kipana
Licha ya kuwakosa Viktor Gyokeres, Kai Havertz na Gabriel Jesus, mabadiliko aliyoyafanya Arteta kwa kuwatambulisha mchezoni Noni Madueke na Gabriel Martinelli yalitosha kuimaliza Bayern.
Wakitokea benchi, Madueke alifunga bao lake la kwanza akiwa Arsenal, wakati Martinelli naye aliingia kambani kufikisha mabao manne kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Habari njema ni kwamba wakati nahodha wa kikosi, Martin Odegaard, akiwa amerejea, Gyokeres na Havertz nao wanaendelea vizuri katika majeraha hayo.
Ni zamu yao ubingwa?
Arsenal haijawahi kunyuakua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Si tu ubingwa, bali pia ni mara moja tu klabu hiyo imeweza kufika fainali, ambapo walifungwa mabao 2-1 na Barcelona mwaka 2006.
Kwa upande mwingine, licha ya kiwango bora katika miaka ya hivi karibuni, Arsenal haijachukua ubingwa wa Ligi Kuu ya England tangu msimu wa 2003-04. Miaka 21 iliyopita.
Kama hiyo haitoshi, Washika Bunduki hawana taji lolote kubwa kwenye kabati lao tangu walipokuwa mabingwa wa FA mwaka 2020.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img