LONDON, Uingereza
WALIKUWEPO Kombe la Dunia mwaka 2006 na sasa wanajiandaa kushiriki fainali za mwakani wakiwa miongoni mwa wachezaji wenye umri mkubwa zaidi. Ni miaka 20 imepita tangu walipocheza michuano hiyo kule Ujerumani.
Ni akina nani hao? Wana umri gani kuelekea mashindano hayo yatakayofanyika Marekani, Canada na Mexico? Na je, watawakilisha mataifa yapi? Endelea kusoma makala haya.
Luka Modric (Croatia)
Croatia imefuzu fainali za mwakani na hii itakuwa mara ya tano kwa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 40, ambaye kwa sasa anakipiga AC Milan, kucheza Kombe la Dunia.
Tangu alipoanza kuitumikia timu ya taifa, Modric amekosa mara moja pekee (2010) kushiriki fainali za Kombe la Dunia. Alikuwa na mchango mkubwa kikosini wakati timu hiyo ilipofika fainali mwaka 2018.
Lionel Messi (Argentina)
Msimu uliopita wa Kombe la Dunia, 2018, aliiongoza timu yake ya taifa ya Argentina kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia akiwa nahodha wa kikosi.
Messi alikuwa benchi kwa dakika zote za mchezo wa robo fainali mwaka 2006 na sasa ana umri wa miaka 38, huku Argentina ikiwa imeshakata tiketi ya kushiriki fainali za mwakani.
Cristiano Ronaldo (Ureno)
Katika fainali za mwaka 2006, nyota huyo raia wa Ureno alifunga bao moja pekee, huku tukio lake la kugombana na Wayne Rooney likizua gumzo kwenye vyombo vya habari duniani kote.
Lilikuwa ni bao lake la 12 lakini sasa ndiye mfungaji bora wa muda wote wa timu ya taifa akiwa na mabao 143. Ana umri wa miaka 40 na amekuwa nahodha wa kikosi kwa miaka 17.
Sergio Ramos (Hispania)
Akiwa na umri wa miaka 21 tu, tayari Ramos alikuwa mchezaji muhimu katika safu ya ulinzi ya Hispania wakati wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2006.
Aliiongoza Hispania kutwaa Kombe la Dunia mwaka 2010. Ni suala la kusubiri na kuona kama atakwenda Marekani, ikizingatiwa kuwa aliondoka katika soka la Ulaya na sasa anakipiga Ligi Kuu ya Mexico akiwa na umri wa miaka 39.
Guillermo Ochoa (Mexico)
Mlinda mlango huyo amekuwa chaguo la kwanza katika kikosi cha timu ya taifa ya Mexico kwa miaka mingi, ikiwamo wakati wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2006.
Katika ngazi ya klabu, amepita Ajaccio, Malaga, Granada, Standard Liege, Salernitana, na sasa anaitumikia AEL Limassol ya Mexico akiwa na umri wa miaka 40.
Lukasz Fabianski (Poland)
Alishiriki fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2006 akiwa kinda anayejifunza kutoka kwa aliyekuwa kipa namba moja wa timu ya taifa ya Poland, Artur Boruc.
Fabianski alistafu mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kutemwa na West Ham United lakini bado aliitwa katika kikosi cha Poland, licha ya umri wake wa miaka 41.
Published:


