LONDON, Uingereza
WAKATI mwingine, mambo huwa hayaendi kama yalivyotarajiwa, hasa katika soko la usajili wa wachezaji wa soka barani Ulaya.
Kwa ufupi, wapo wanasoka waliosajiliwa kwa fedha nyingi lakini wakashindwa kuendeleza makali waliyokuwa nayo katika klabu walizotoka. Si ajabu!
Wirtz & Isak
Miezi miwili tu iliyopita, Liverpool iliwasa Florian Wirtz na Alexander Isak kutoka Bayer Leverkusen na Newcastle United. Wirtz aliigharimu Liverpool kiasi cha Pauni milioni 116, wakati usajili wa Isak ulikuwa wa Pauni milioni 130.
Hata hivyo, nyota hao wameshindwa kufikia matarajio makubwa waliyokuwa nayo mabosi wa Liverpool. Katika Ligi, Wirtz raia wa Ujerumani hajafunga bao wala kutoa ‘asisti’. Isak hajafunga, ingawa ana asisti moja.
Jack Grealish (Man City)
Manchester City walitumia Pauni milioni 100 kumng’oa Leicester City, wakati huo Grealish akiwa mchezaji wa kiwango cha juu.
Hata hivyo, misimu miwili tu baadaye, Grealish alishindwa kuwika na aliingia mara 20 pekee katika kikosi cha kwanza. Aliposajiliwa Jeremy Doku mwaka 2023, ukawa mwisho wake wa kupata nafasi. Akahamia Everton majira ya kiangazi, mwaka huu.
Romelu Lukaku (Chelsea)
Baada ya kiwango kizuri akiwa Inter Milan, ambapo alifunga mabao 64 katika mechi 95, Lukaku alisajiliwa na Chelsea kwa ada ya Pauni milioni 97.5 mwaka 2021.
Licha ya kufunga mabao manne katika mechi nne za mwanzo, Mbelgiji huyo alianza kupotea. Kilichofuata ni mabao 15 pekee katika michezo 44, kabla ya kuondoka zake Stamford Bridge.
Paul Pogba (Man United)
Usajili uliogharimu Manchester United kitita cha Pauni milioni 89 mwaka 2016. Ni baada ya Pogba kuondoka Old Trafford akiwa mchezaji huru mwaka 2012.
Licha ya fedha nyingi zilizotumika kumsajili, msimu pekee ambao kiungo huyo alikuwa mchezaji wa kiwango cha juu ni 2018-19, ambapo alifunga mabao 13 ya Ligi Kuu.
Aanthony (Man United)
Pauni milioni 82 zilitumika kumpeleka Old Trafford akitokea Ajax mwaka 2022, ukiwa ni usajili wa kocha aliyewahi kumnoa katika kikosi hicho, Erik ten Hag.
Tofauti na kiwango bora alichokuwa nacho Ajax, mabao 24 na asisti 22, Anthony hakuweza kung’ara akiwa Man United. Alifunga mabao matatu pekee kwa misimu miwili na nusu aliyokuwa Old Trafford. Alitimkia Real Betis.
Published:


