MUNICH, Ujerumani
KWA miaka ya hivi karibuni, Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) ni kama imepoteza ushawishi wake mbele ya Ligi Kuu ya England (EPL). Kivipi?
Iko hivi; huku Bundesliga ikishindwa kuishawishi wachezaji wenye majina makubwa kujiunga nayo, vipaji vingi vinavyoibuliwa na Ligi hiyo vimekuwa vikikimbilia EPL.
Wakati wa usajili wa kiangazi, mwaka huu, wachezaji zaidi ya 14 walijiunga na klabu za England wakitokea Bundesliga.
Miongoni mwao ni Florian Wirtz, ambaye usajili wake wa Pauni milioni 116.5 akitokea RB Leipzig ulivunja rekodi ya wachezaji wa bei mbaya zaidi kuwahi kununuliwa na Liverpool.
Kwa sasa, wapo wachezaji kadhaa wanaofanya vizuri Bundesliga, ambao nao haitashangaza kuona wakitimkia EPL katika siku za usoni.
Lennart Karl (Bayern Munich)
Kiungo mshambuliaji huyo ana umri wa miaka 17 tu. Ni kinda aliyetokea katika ‘academy’ ya Bayern Munich na sasa ameanza kuaminiwa kwenye timu ya wakubwa.
Miongoni mwa wanaovutiwa na kiwango cha ‘dogo’ huyo ni mshambuliaji wa Bayern, Harry Kane, ambaye amemtabiria kuwa staa wa baadaye.
Yan Diomande (RB Leipzig)
Kiungo wa pembeni mwenye umri wa miaka 19. Nyota huyo wa kimataifa wa Ivory Coast ana mabao matatu na ‘asisti’ tatu katika mechi tatu zilizopita za Leipzig.
Diomande aliyewahi kukataliwa na ‘academy’ ya Rangers wakati fulani wa utoto wake, ameingia kwenye rada za Arsenal, Chelsea, Liverpool, Manchester City, PSG, Barcelona na Real Madrid.
Said El Mala (FC Cologne)
Winga mwenye umri wa miaka 19 katika kikosi cha Cologne. Msimu huu, benchi la ufundi la timu hiyo limempa nafasi ya kucheza mechi 10. Pia, ameitwa katika kikosi cha Ujerumani.
Licha ya kwamba El Mala ameingia kikosi cha kwanza mara tatu pekee katika mechi hizo, ameweza kufunga mabao manne na kutoa ‘asisti’ moja.
Hugo Larsson (Frankfurt)
Huyo ni kiungo mwenye umri wa miaka 21. Alikuwa moto wa kuotea mbali msimu uliopita, kiasi cha kupokea ofa nyingi kutoka kwa klabu tajiri za Ligi Kuu ya Saudi Arabia.
Hata hivyo, ‘mido’ huyo raia wa Sweden aligoma na sasa klabu kadhaa za Ligi Kuu ya England, ikiwamo Liverpool, zimeanza kuimezea mate saini yake.
Assan Ouedraogo (RB Leipzig)
Ana umri wa miaka 19 tu lakini Ouedraogo ni mmoja ya viungo wa kati wanaofanya vizuri kwa sasa Ligi Kuu ya Ujerumani. Ana urefu wa futi 6 na inchi 3.
Leipzig walimnasa Julai, mwaka jana, akitokea Schalke 04. Msimu huu, ameshafunga mabao mawili na kutoa ‘asisti’ nne. Mwezi uliopita, alifunga bao wakati timu yake ya U-21 ya Ujerumani ilipoifunga Ireland.
Luka Vuskovic (Hamburg)
Beki mwenye umri wa miaka 18. Ni nyota wa kimataifa wa Croatia anayecheza kwa mkopo Hamburg akitokea England alikokuwa akiitumikia Tottenham.
Vuskovic ndiye beki alicheza mipira mingi ya juu msimu huu wa Bundesliga. Kama hiyo haitoshi, ametwaa mara mbili tuzo ya Beki Bora wa Mwezi (Septemba na Oktoba).
Nathaniel Brown (Frankfurt)
Mlinzi wa kushoto mwenye umri wa miaka 22. Msimu uliopita, Brown alikuwa na mchango mkubwa kwa Frankfurt, ambapo alifunga mabao matatu na kutoa ‘asisti’ saba.
Kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuzuia na kupandisha mshambulizi, nyota huyo ameingia kwenye rada za Real Madrid, Arsenal na Manchester City.
Antonio Nusa (RB Leipzig)
Akiwa na umri wa mabao 20 kwa sasa, winga huyo ni tishio Bundesliga. Staa wa timu ya taifa ya Norway, Erling Haaland, amemtabiria makubwa raia mwenzake huyo.
Mwaka 2022, Nusa, ambaye anafananishwa na Neymar, aliingia kwenye historia ya kuwa mchezaji wa pili mwenye umri mdogo zaidi (miaka 17 na siku 149) kufunga bao katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ibrahim Maza (Bayern Munich)
Kiungo mshambuliaji raia wa Algeria mwenye umri wa miaka 19. Licha ya uchanga wake, ndiye aliyeibuka nyota wa mchezo katika mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Benfica.
Ni baada ya mchezo huo, Maza aliendeleza makali yake kwa kupasia nyavu mara mbili katika ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Heidenheim. Anafananishwa na Florian Wirtz.
Castelo Lukeba (RB Leipzig)
Beki wa kati mwenye umri wa miaka 22. Leipzig ilimsajili kuziba pengo la Josko Gvardiol aliyeondoka klabuni hapo na kutimkia Manchester City.
Lukeba raia wa Ufaransa, amekuwa akiipa wakati ngumu Leipzig pindi anapokosekana uwanjani, kama ilivyokuwa katika mchezo uliopita walipotandikwa mabao 3-1 na Hoffenheim.
Can Uzun (Frankfurt)
Kiungo mshambuliaji huyo ana umri wa miaka 20. Baada ya Frankfurt kuwauza kwa Ekitike na Marmoush, sasa Uzun ndiye staa mpya klabuni hapo.
Nyota huyo raia wa Uturuki, ambaye anawaniwa na Tottenham, aliuanza kwa kasi msimu huu, ambapo alifunga mabao matano katika mechi tano. Kwa sasa, ameongeza ‘asisti’ nne.
Published:


